Swali 11: Mtu akikosa swalah ya mkusanyiko msikitini kisha akaswali nyumbani kwake kama imamu na mke wake – je, anapata fadhilah za ujira wa swalah ya mkusanyiko[1]?

Jibu: Ni lazima kwa muumini kuharakisha kuswali msikitini pamoja na mkusanyiko. Amesema (Subhaanah):

حَافِظُوا عَلَى الصَّلَوَاتِ وَالصَّلَاةِ الْوُسْطَىٰ

“Zihifadhini swalah [za kila siku] na [khaswa] swalah ya katikati.”[2]

وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَارْكَعُوا مَعَ الرَّاكِعِينَ

“Simamisheni swalah na toeni zakaah na rukuuni pamoja na wanaorukuu.”[3]

قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ

“Hakika wamefaulu waumini; ambao katika swalah zao ni wenye kunyenyekea.”[4]

Mpaka aliposema:

الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Ambao watarithi [Pepo] ya al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu.”[5]

 “Yeyote atakayesikia adhaana na asiitikie basi hana swalah isipokuwa akiwa na udhuru.”[6]

Akaulizwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa): “Ni udhuru upi?” Akasema: “Khofu au maradhi.”

Katika “as-Swahiyh” ya Muslim pia amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema: “Bwana mmoja kipofu alisema: “Ee Mtume wa Allaah! Sina kiongozi wa kuniongoza msikitini. Je, ninayo ruhusa ya kuswali nyumbani kwangu?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza: “Je, wasikia wito wa swalah?” Akasema: “Ndio.” Akasema: “Basi imewajibika.”[7]

Zipo Hadiyth nyingi zenye maana kama hii.

Atakayepitwa na mkusanyiko na akaswali akiwa imamu pamoja na mke wake hapana neno. Kunatarajiwa juu yao fadhilah za mkusanyiko akiwa ni mwenye kupewa udhuru. Lakini hata hivyo asimame nyuma yake na asisimame sambamba naye.

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (12/68-69).

[2] 02:238

[3] 02:43

[4] 23:01-02

[5] 23:01-11

[6] Ibn Maajah (785).

[7] Muslim (653) na an-Nasaa´iy (850).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam Swalaat-il-Jumu´ah wal-Jamaa´ah, uk. 37-38
  • Imechapishwa: 26/11/2021