11. Hukumu ya swawm zilizopita


Muislamu! Jifunze baadhi ya hukumu zinazohusu na kulipa kwa ambaye hakufunga Ramadhaan.

Kila ambaye analazimika kulipa siku zilizompita katika Ramadhaan basi analazimika kufanya hivo kabla ya Ramadhaan inayofuata. Kwa mfano ikiwa mtu alipitwa na siku mbili, tatu au nne ni wajibu kuzilipa siku hizo. Lakini haimlazimu kuzilipa kwa mfululizo. Endao atafanya hivo ndio bora zaidi. Anaweza kuchelewesha kulipa mpaka Sha´baan. Ikiwa kutaingia Ramadhaan nyingine kabla ya kulipa siku zake anapata dhambi iwapo atakuwa hana udhuru. Atatakiwa kuzilipa siku hizo pamoja vilevile na kulisha kwa kila siku moja masikini. Wengi katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamefutu hivyo. Kiwango cha chakula ni Swaa´ moja, takriban 1 ½  kg, ya chakula cha mji kilichozoeleka sana ambacho watapewa masikini hata kama atakuwa ni masikini mmoja tu.

Iwapo mtu atakuwa amechelewesha kwa udhuru kama maradhi au safari, kinachomlazimu ni kulipa siku hizo tu. Hahitajii kulisha kutokana na ujumla wa maneno ya Allaah (Subhaanah):

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo.”[1]

TANBIHI

Muislamu akikata swawm katika Ramadhaan kwa sababu ya maradhi na akafa hakuna kinachomlazimu si kulipa wala kulisha, kwa kuwa ni mwenye kupewa udhuru na hakuweza kulipa.

Hali kadhalika inahusu safiri endapo atakufa katika safari yake au papo hapo baada ya kufika katika mji wake. Katika hali hii haimlazimu kumlipia siku hiyo wala kuwalisha masikini chakula. Kwa kuwa huyu pia Kishari´ah ana udhuru.

Kuhusiana na ambaye atapona na akapuuza kuzilipa siku zake mpaka akafariki au akarudi kutoka katika safari yake na akapuuza kuzilipa siku zake mpaka akafariki, imewekwa katika Shari´ah mawalii katika nduguze wamlipie siku hizo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Atayekufa na juu yake  ana swawm, walii wake ndiye atamfungia.”[2]

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amepokea kwa mlolongo wa wapokezi Swahiyh kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba kuna mwanamke alimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama anatakiwa kulipa siku za mama yake za Ramadhaan? Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akajibu:

“Unaonaje lau mama yako angelikuwa na deni ungelimlipia nalo? Deni la Allaah lina haki zaidi kulipwa.”[3]

Hadiyth hii, Hadiyth ilio kabla yake na Hadiyth zilizo na maana yazo zote zinafahamisha kuwa maiti anatakiwa kulipiwa swawm sawa ikiwa ni swawm ya nadhiri, swawm ya Ramadhaan au kafara. Haya ndio maoni sahihi ya wanachuoni.

Ikiwa haiwezekani kumfungia basi mtu anatakiwa kumtolea chakula kutoka katika mirathi ya maiti. Kwa kila siku iliyompita kutatolewa Swaa´ moja, takriban 1 ½ kg, kumpa masikini. Hali kadhalika inamuhusu mtumzima na mgonjwa ambaye maradhi yake hayatarajiwi kupona. Vivyo hivyo mwenye hedhi na nifasi wakipuuza kulipa siku zao mpaka wakafariki. Iwapo hakutokuwa mwenye kuwafungia kutolewe chakula kumpa masikini kwa kila siku moja. Ambaye hakuacha mirathi ambayo chakula kitachukuliwa kutoka humo haimlazimu kitu. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah hakalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya uwezo wake.”[4]

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

“Basi mcheni Allaah muwezavyo.”[5]

Ninamuomba Allaah kwa majina Yake mazuri na sifa Zake kuu atuwafikishe sisi na nyinyi katika elimu yenye manufaa na matendo mema, atukinge sisi sote kutokamana na uovu wa nafsi zetu na matendo yetu maovu na atuongoze sote katika njia iliyonyooka. Ninamuomba Allaah atujaalie kushindana katika kila kheri na atukinge na kila shari. Ninamuomba Allaah awaongoze watawala wetu katika kila kheri, ainusuru dini Yake kupitia wao, awatengenezee matangamano yao, awasaidie kwa kila kheri na awakinge kwa kila shari. Ninamuomba Allaah awawafikishe wenye mamlaka wote katika yale anayoyaridhia na katika yale yenye manufaa kwa watu na miji. Ninamuomba Allaah (Subhaanah) azitengeneze hali za waislamu kila mahali, awatawalishie watawala bora, awatengeneze viongozi wao na awatunuku uelewa na kuwa na msimamo  katika dini. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na yukaribu.

Swalah na salaam zimwendee mja na Mtume Wake, Mtume wetu Muhammad, kizazi chake, Maswahabah wake na wenye kuwafuata kwa wema.

[1] 02:185

[2] al-Bukhaariy (1952) na Muslim (1147).

[3] Ahmad (2005) na Abu Daawuud (3310). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Abiy Daawuud” (2831). Hadiyth kama hiyo inapatikana katika al-Bukhaariy (1953) na Muslim (1148) tofauti muulizaji ni mwanaume.

[4] 02:286

[5] 64:16