Hadiyth ya sita

6- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia: “Nilikuwa na deni la swawm ya Ramadhaan na siwezi kuilipa isipokuwa katika Sha´baan.”

Maana ya kijumla:

“´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) anataja wakati mwingine anakuwa na deni la swawm ya Ramadhaan na kutokana na Mtume (Radhiya Allaahu ´anhaa) alivyokuwa anampenda na kuchunga matangamano mazuri yaliokuwa kati yao, basi anachelewesha kulipa mpaka katika Sha´baan. Kwa sababu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifunga sana katika Sha´baan. Akilijua hilo na akimkubalia.

Faida zinazochukuliwa kutoka katika Hadiyth:

1- Inafaa kuchelewesha kulipa deni la Ramadhaan mpaka katika Sha´baan kukiwa kuna udhuru wa kufanya hivo.

2- Bora ni kuharakisha kulipa ikiwa hakuna udhuru. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amebainisha udhuru wake katika hilo.

3- Haijuzu kuchelewesha deni mpaka ikaingia Ramadhana ya pili. Wanachuoni wametofautiana juu ya uwajibu wa kutoa kafara kwa yule aliyechelewesha mpaka kukaingia Ramadhaan ya pili. Madhehebu ya Hanaabilah wanasema kwamba ni wajibu kwake kutoa kafara akichelewesha pasi na udhuru.

4- Namna ambavyo ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alivyokuwa akitangamana kwa uzuri na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tunamuomba Allaah awajaalie wake zetu kumuiga.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-´Allaam Sharh ´Umdat-il-Ahkaam, uk. (01/130-131)
  • Imechapishwa: 08/06/2018