11. Elekeza uso wako katika dini yenye imani safi na iliyotakasika

Allaah (Ta´ala) amesema:

فَأَقِمْ وَجْهَكَ لِلدِّينِ حَنِيفًا ۚ فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا ۚلَا تَبْدِيلَ لِخَلْقِ اللَّـهِ ۚ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ

“Basi elekeza uso wako katika dini yenye imani safi na iliyotakasika, imani hiyo ndio maumbile Allaah aliyowaumbia watu [wote] – hakuna mabadiliko katika uumbaji wa Allaah! Hivyo ndio dini iliyonyooka sawasawa, lakini watu wengi hawajui. (30:30)

وَوَصَّىٰ بِهَا إِبْرَاهِيمُ بَنِيهِ وَيَعْقُوبُ يَا بَنِيَّ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ لَكُمُ الدِّينَ فَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

“Na Ibraahiym akawausia hayo wanawe na [kadhalika] Ya’quub [akawaambia]: “Enyi wanangu! Hakika Allaah amekuchagulieni nyinyi dini; hivyo basi msife isipokuwa nyinyi ni waislamu.” (02:132)

ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا ۖ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ

“Kisha Tukakufunulia Wahy kwamba fuata imani ya Ibraahim iliyo safi na kutakasika na hakuwa miongoni mwa washirikina.” (16:123)

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika kila Mtume ana msaidizi katika Mitume na mimi msaidizi wangu katika wao ni baba yangu na Khaliyl wa Allaah Ibraahiym.” Halafu akasoma:

إِنَّ أَوْلَى النَّاسِ بِإِبْرَاهِيمَ لَلَّذِينَ اتَّبَعُوهُ وَهَـٰذَا النَّبِيُّ وَالَّذِينَ آمَنُوا ۗوَاللَّـهُ وَلِيُّ الْمُؤْمِنِينَ

“Hakika watu waliokaribu zaidi kwa Ibraahiym ni wale waliomfuata, kama mfano wa Nabii huyu na wale walioamini. Na Allaah ni Mlinzi wa waumini.”[1] (03:68)

Ameipokea at-Tirmidhiy.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Uislamu ulianza ni kitu kigeni na utarudi kuwa kitu kigeni kama ulivyoanza. Hivyo Twuubaa kwa wale wageni!”

Ameipokea Muslim.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah hatazami miili yenu wala mali zenu; anatazama nyoyo zenu na matendo yenu.”[2]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kutoka kwa Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mimi nitakutangulieni kwenye hodhi. Wanaume katika Ummah wangu watanyanyuliwa kwangu na pindi ninapoenda kuwachukua, watawekwa mbali na mimi ambapo nitasema: “Ee Mola! Wafuasi wangu!” Kusemwe: “Hakika wewe hujui waliyozusha baada yako.”[3]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninatamani lau tungeliwaona ndugu zetu.” Waseme: “Ee Mtume wa Allaah! Kwani sisi sio ndugu zako?” Akasema: “Nyinyi ni Maswahabah zangu. Ndugu zangu ni wale ambao bado hawajaja.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Vipi utamjua ni nani katika Ummah wako ambaye bado hajaja?” Akajibu: “Mnaonaje lau mtu atakuwa na farasi mwenye baka jeupe kati ya farasi weusi, hatomjua farasi wake?” Wakasema: “Ndio, ee Mtume wa Allaah.” Akasema: “Watakuja wakiwa na mabaka ya kung´aa yanayotokamana na wudhuu´. Nitawatangulia katika hodhi. Hata hivyo kuna wanamme wataofukuzwa mbali na hodhi yangu siku ya Qiyaamah kama anavyofukuzwa ngamia aliyepotea. Ninawaita, lakini kutasemwa: “Walibadilisha baada yako”, kisha niseme: “Tokomeeni! Tokomeeni!”[4]

Katika al-Bukhaariy imekuja:

“Nitapokuwa nimesimama katika umati wa watu. Pindi nitapowajua nao wanijue atajitokeza mtu kati yetu na kusema: “Njooni!” Niseme: “Kuelekea wapi?” Aseme: “Ninaapa kwa Allaah! Kuelekea Motoni.” Niseme: “Kwani wana nini?” Aseme: “Waliritadi baada yako.” Halafu kuje umati mwingine”, na useme hali kadhalika. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Wachache sawa na idadi ya ngamia walioachwa ndio wataifikia.”[5]

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Nitasema kama alivyosema mja mwema:

وَكُنتُ عَلَيْهِمْ شَهِيدًا مَّا دُمْتُ فِيهِمْ ۖ فَلَمَّا تَوَفَّيْتَنِي كُنتَ أَنتَ الرَّقِيبَ عَلَيْهِمْ ۚ وَأَنتَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ

“Na nilikuwa juu yao shahidi wakati nilipokuwa nao, lakini uliponipaisha juu ulikuwa Wewe ndiye Mwenye kuchunga juu yao; na Wewe juu ya kila jambo ni Mwenye kushuhudia.” (05:117)

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna mtoto yeyote isipokuwa huzaliwa katika maumbile. Baada ya hapo wazazi wake ndio humfanya kuwa myahudi, mnaswara au mwabudia moto. Ni kama ambavo mnyama huzaa mnyama mzima; je, mtahisi kuwa hana pembe mpaka nyinyi ndiye mumwondoshe pembe?”  Kisha Abu Hurayrah akasoma:

فِطْرَتَ اللَّـهِ الَّتِي فَطَرَ النَّاسَ عَلَيْهَا

“… imani hiyo ndio maumbile Allaah aliyowaumbia watu wote…” (30:30)

Hudhayfah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Watu walikuwa wakimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu mambo ya kheri na mimi nikimuuliza kuhusu mambo ya shari kwa kuchelea yasije kunipata. Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tulikuwa katika kipindi cha kikafiri na shari na Allaah akatuletea kheri hii. Je, kuna shari baada ya kheri hii?” Akajibu: “Ndio.” Nikasema: “Je, kuna kheri baada ya shari hiyo?” Akajibu: “Ndio, na itakuwa na moshi.” Nikamuuliza: “Ni upi moshi wake?” Akajibu: “Ni watu wenye kufuata isiyokuwa njia na uongofu wangu. Kuna mambo utayokubaliana nayo na mengine utayapinga.” Nikasema: “Kuna shari baada ya kheri hiyo?” Akasema: “Ndio, fitina ya upofu na walinganizi katika milango ya Motoni. Yule mwenye kuwaitikia wanamtupa humo.” Nikasema: “Ee Mtume wa Allaah! Tueleze nao.” Akasema: “Ni watu wanaotokamana na sisi na wanazungumza lugha yetu.” Nikauliza: “Unaniamrisha nini nikikutana na hilo?” Akasema: “Shikamana na mkusanyiko wa waislamu na kiongozi wao.” Nikasema: “Vipi kukiwa hakuna mkusanyiko wala kiongozi?” Akasema: “Jiepushe na hayo makundi yote hata kama utahitajia kuuma mzizi wa mti mpaka yakufikie mauti.”[6]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim ambaye amezidisha:

“Kuna nini baadaye?” Akasema: “Kisha atajitokeza ad-Dajjaal. Atakuwa na mto na moto. Atayetumbukia kwenye moto wake itamuwajibikia kulipwa ujira wake na madhambi yake kufutwa. Na yule mwenye kutumbukia kwenye pepo yake itamuwajibikia kuadhibiwa.” Nikasema: “Kuna nini baadaye?” Akasema: “Halafu kunakuja Qiyaamah.”[7]

Abul-´Aaliyah amesema:

“Jifunzeni Uislamu. Mtapojifunza, msiupe mgongo. Lazimianeni na njia iliyonyooka, kwani hakika ndio Uislamu. Msende kinyume na njia kuliani na kushotoni. Lazimianeni na Sunnah za Mtume wenu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na tahadharini na matamanio haya.”

Yazingatie maneno haya ya Abul-´Aaliyah – ni matukufu kiasi gani! Tambua zama zake ambapo akitahadharisha matamanio ambayo yule mwenye kuyafuata anakuwa ameupa Uislamu mgongo. Ameufasiri Uislamu kuwa ni Sunnah na khofu yake ilikuwa kwa Taabi´uun mabingwa wasiende kinyume na Qur-aan na Sunnah. Hapo ndipo itakubainikia maana ya maneno ya Allaah:

إِذْ قَالَ لَهُ رَبُّهُ أَسْلِمْ ۖ قَالَ أَسْلَمْتُ لِرَبِّ الْعَالَمِينَ

“Pindi Mola Wake alipomwambia: “Jisalimishe!” Akajibu: “Nimejisalimisha kwa [Allaah], Mola wa walimwengu.” (02:131)

na:

وَوَصَّىٰ بِهَا إِبْرَاهِيمُ بَنِيهِ وَيَعْقُوبُ يَا بَنِيَّ إِنَّ اللَّـهَ اصْطَفَىٰ لَكُمُ الدِّينَ فَلَا تَمُوتُنَّ إِلَّا وَأَنتُم مُّسْلِمُونَ

“Na Ibraahiym akawausia hayo wanawe na [kadhalika] Ya’quub [akawaambia]: “Enyi wanangu! Hakika Allaah amekuchagulieni nyinyi dini; hivyo basi msife isipokuwa nyinyi ni waislamu.” (02:132)

na:

وَمَن يَرْغَبُ عَن مِّلَّةِ إِبْرَاهِيمَ إِلَّا مَن سَفِهَ نَفْسَهُ ۚ وَلَقَدِ اصْطَفَيْنَاهُ فِي الدُّنْيَا ۖ وَإِنَّهُ فِي الْآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ

“Na nani atakayejitenga na imani ya Ibraahiym isipokuwa anayeitia nafsi yake upumbavu? Na kwa hakika Tumemteua duniani, naye Aakhirah ni miongoni mwa waja wema.” (02:130)

Izingatie misingi hii mikubwa ambayo ndio misingi ya misingi na ambayo watu wameghafilika nayo. Kwa kuielewa basi itabainika maana ya Hadiyth katika mlango huu na mingineyo.

Kuhusiana na yule mwenye kuisoma ni mamoja hii na mingineyo na huku anajiaminisha kuwa hayawezi kumfika na anafikiria kuwa yanawahusu watu waliokuwepo hapo kale wakatokomea, basi Allaah yuwasema:

أَفَأَمِنُوا مَكْرَ اللَّـهِ ۚ فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ

“Je, wameaminisha njama za Allaah? Basi hawaaminishi njama za Allaah isipokuwa watu wenye kukhasirika.” (07:99)

Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Siku moja Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitupigia msitari kwenye ardhi kisha akasema: “Hii ni njia ya Allaah.” Halafu akapiga vimisitari kuliani na kushotoni kisha akasema: “Hivi ni vichochoro. Kuna Shaytwaan mwenye kuita katika kila kichochoro.” Halafu akasoma:

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Hii ndio njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate vichochoro [vinginevyo]; vikakufarikisheni na njia Yake!”[8] (06:153)

[1] at-Tirmidhiy (2995), al-Bazzaar (5/345) na al-Haakim (2/320).

[2] Muslim (2564).

[3] al-Bukhaariy (7049) na Muslim (2297).

[4] Muslim (249).

[5] al-Bukhaariy (6587).

[6] al-Bukhaariy (3606) na Muslim (1847).

[7] ´Abdur-Razzaaq katika ”al-Muswannaf” (11/367), al-Marwaziy katika ”as-Sunnah”, uk. 13, al-Laalakaa’iy katika ”Sharh Usuwl I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah (1/56) na Abu Nu´aym (2/218).

[8] an-Nasaa’iy (6/343), Ahmad (1/435), ad-Daarimiy (202) na al-Bazzaar (57113).

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwl-ul-Islaam, uk. 32-38
  • Imechapishwa: 23/10/2016