15. ´Aqiydah sahihi juu ya watawala wa waislamu

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaitakidi kuwa Allaah (Ta´ala) amewawajibishia waumini kuwatii watawala wao katika yote yasiyokuwa maasi. Wanaamini maana ya maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) iliyotajwa katika Hadiyth ya ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anh):

“Sikiliza na utii katika kipindi chako kizito na chepesi, katika unayoyapenda na unayoyachukia hata kama watapendelea dhidi yako mambo ya kidunia pasi na kukupatia haki yako, hata kama watachukua mali yako na kupiga mgongo wako, midhali haihusiani na maasi.”

Ameipokea Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake kwa cheni ya wapokezi nzuri. Msingi wake ni kwa al-Bukhaariy na Muslim.

Wanaonelea kuwa ni haramu kuwafanyia uasi watawala, hata kama watakuwa wakandamizaji na wenye kudhulumu, midhali hawajaona kufuru ya wazi ambayo kwayo wana dalili kutoka kwa Allaah. Hayo ni kutokana na yale aliyosema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wabora wa viongozi wenu ni wale mnaowapenda na wao wanakupendeni na wale mnaowaombea du´aa na wao wanakuombeeni du´aa. Waovu wa viongozi wenu ni wale mnaowachukia na wao wanakuchukieni na mnawalaani na wao wanakulaanini.” Kukasemwa: “Ee Mtume wa Allaah! Je, tusipambane nao kwa panga?” Akasema: “Hapana, muda wa kuwa wanasimamisha swalah. Mtapoona kitu kutoka kwa watawala wenu mnachokichukia, basi chukieni kitendo chake na wala msinyanyue mkono kutoka katika utiifu.”

Katika matamshi mengine imekuja:

“Yule aliye na mtawala juu yake na akaona anafanya kitu katika kumuasi Allaah, basi na achukie kitendo kinachomuasi Allaah na wala asinyanyue mkono kutoka katika utiifu.”

Ameipokea Muslim kutoka kwa ´Awf bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh).

Yule mwenye kutoka katika Mkusanyiko, basi Shari´ah itamuadhibu adhabu kali duniani na Aakhirah kutegemea na ukubwa wa dhambi yake. Miongoni mwa hayo ni kwamba yule mwenye kufa baada ya kutoka katika utiifu na akafarikiana na Mkusanyiko, basi amekufa kifo cha kipindi cha kikafiri. Mtu asiulizie juu ya mtu mwenye kufarikiana na Mkusanyiko kutokana na ukubwa wa dhambi yake. Mwenye kufarikiana na Mkusanyiko basi hana hoja yoyote mbele ya Allaah (Ta´ala) siku ya Qiyaamah. Yule mwenye kufarikiana na Mkusanyiko shaytwaan yuko pamoja naye bega kwa bega. Mwenye kufarikiana na Mkusanyiko basi damu yake ni halali.

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaonelea kuwa ni jambo zuri na lenye kusifika kumuombea mtawala kwa Allaah juu ya mafanikio na usalama. Nayo ni alama yenye kuonesha kuwa mtu ni katika Ahl-us-Sunnah, kama alivyosema Imaam al-Barbahaariy katika kitabu “Sharh-us-Sunnah”:

“Ukimuona mtu anaomba du´aa dhidi ya mtawala, basi tambue kuwa ni katika watu wenye kufuata matamanio. Na ukimuona mtu anamuombea du´aa mtawala juu ya kutengemaa, basi tambua kuwa ni katika watu wa Sunnah – Allaah akitaka.”

Fudhwayl bin ´Iyaadhw amesema:

“Lau mimi ningelikuwa na du´aa yenye kuitikiwa basi nisingelimuombea mwengine asiyekuwa mtawala. Tumeamrishwa kuwaombea kutengemaa na hatukuamrishwa kuomba dhidi yao ingawa watakuwa ni wakandamizaji na wenye kudhulumu. Ule ukandamizaji na dhuluma zao ni jambo linawapata wao wenyewe na waislamu pia na kutengemaa kwao ni jambo linawapata wao wenyewe na waislamu pia.”

Imaam as-Swaabuuniy amesema katika “´Aqiydat-us-Salaf wa Aswhaab-il-Hadiyth”:

“Wanaonelea kuwaombea kutengemaa, mafanikio na uongofu.”

Wanaona wale wakubwa wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wameafikiana juu ya kwamba ni haramu kuwatukana. Anas bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Wakubwa wetu katika Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wametukataza kwa kusema: “Msiwatukane viongozi wenu, msiwafanyie ghushi na wala msiwachukie. Mcheni Allaah na kuweni na subira, kwani hakika jambo linakaribia.”

Ameipokea Ibn Abiy ´Aaswim katika “as-Sunnah” na wengineo.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mu´taqad as-Swahiyh, uk. 91-94
  • Imechapishwa: 22/06/2020