109. Ihsaan kati ya mtu na wenzake


2- Kuhusu Ihsaan kati ya mja na viumbe wenzake ni kule yeye kuwatendea wema na kujizuia kuwadhuru. Hayo yanakuwa kwa njia ya kumlisha mwenye njaa, kumvisha aliyeuchi, kumsaidia muhitaji kutokana na cheo chako na kumpitia mbele yule anayehitajia kuombewa. Kufanya wema kwa aina zake zote, kumkirimu mnyonge na jirani. Hakuna kinachotoka kwako kwenda kwa jirani yako isipokuwa kheri tupu na pia ujizuie na kumdhuru. Kwa msemo mwingine kusitoke kwako maudhi na madhara kwake wala juu ya mwengine.

Miongoni mwa watu wako ambao hakutoki kwao isipokuwa madhara matupu. Miongoni mwa  watu wengine wako ambao hakutoki kwao isipokuwa kheri na madhara. Miongoni mwa  watu wengine wako ambao hakutoki kwao isipokuwa kheri tupu. Hawa ndio wako katika ngazi za juu kabisa. Kuwatendea watu kheri na kujizuia na kuwadhuru ndio Ihsaan kwa watu:

وَأَحْسِنُوا ۛ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ

“Fanyeni ihsaan, kwani hakika Allaah anapenda wafanyao ihsaan.[1]

Mpaka wanyama mtu anatakiwa kuwatendea wema kwa njia ya kuwaandalia yale wanayohitajia, kutowadhuru na kuwafanyia urafiki. Huku ndio kufanyia wema wanyama. Hata yule ambaye anastahiki kuuliwa usimuadhibu. Bali unatakiwa kumuua kifo kizuri na cha kumpumzisha. Yule ambaye amestahikiwa kulipiziwa kisasi na adhabu ya Kishari´ah basi unatakiwa kumfanyia kwa urafiki. Usimkatekate viungo, usimwadhibu wala usimdhuru. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Hakika Allaah amefaradhisha wema juu ya kila kitu. Hivyo basi, mtapoua basi ueni kwa uzuri na mtapochinja basi chinjeni kwa uzuri.”[2]

Haya yanahusu kisasi au mengineyo ambayo yanalazimu adhabu ya Kishari´ah.

Mtapochinja – Bi maana mtapochinja wanyama wa kula.

Basi ueni kwa uzuri:

“Mmoja wenu anoe vizuri kifaa chake na apumzishe kichinjwa chake.”

Unatakiwa kuwafanyia wema mpaka wanyama:

Allaah alimsamehe mwanamke mzinzi wa wana wa israaiyl kwa sababu ya mwanamke huyo kumpa maji mbwa ambaye anatoa ulimi nje kwa sababu ya kiu ambapo akamtolea shukurani mbele ya Allaah na ikawa ni sababu ya Allaah kumsamehe dhambi yake[3]. Isitoshe ni dhambi kubwa ya umalaya. Allaah akamsamehe kwa sababu ya kumpa maji mnyama huyu mwenye kiu. Tusemeje mbali na mbwa endapo mtu atawafanyia wema waislamu wote au akawafanyia wema wanadamu wote kukiwemo makafiri. Ukimfanyia wema basi Allaah (Jalla wa ´Alaa) anakushukuru kwa wema huo. Amesema (Ta´ala):

وَأَحْسِنُوا ۛ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُحْسِنِينَ

“Fanyeni ihsaan, kwani hakika Allaah anapenda wafanyao ihsaan.

[1] 02:195

[2] Muslim (1955).

[3] al-Bukhaariy (3467) na Muslim (2245).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 227-229
  • Imechapishwa: 28/01/2021