Baada ya hapo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anafanya Tasliym upande wa kulia kwake kwa kusema:

السلام عليكم و رحمة الله

“Amani na rehema ya Allaah iwe juu yenu.”

kiasi cha kwamba mtu alikuwa anaweza kuona weupe wa shavu lake la kulia. Kisha anafanya Tasliym upande wake wa kushoto na kusema:

السلام عليكم و رحمة الله

“Amani na rehema ya Allaah iwe juu yenu.”

kiasi cha kwamba mtu alikuwa anaweza kuona weupe wa shavu lake la kushoto[1].

Wakati fulani (Swalla Allaahu ´alayhiwa sallam) alikuwa anaweza kusema katika Tashahhud ya kwanza:

السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

“Amani na rehema na baraka za Allaah ziwe juu yenu.”[2]

Mara husema:

السلام عليكم و رحمة الله

“Amani na rehema ya Allaah iwe juu yenu.”

upande wa kulia na husema:

السلام عليكم

“Amani ya Allaah iwe juu yenu.”

peke yake upande wa kushoto[3].

Nyakati fulani (Swalla Allaahu ´alayhiwa sallam) hufanya Tasliym moja peke yake na husema:

السلام عليكم

“Amani ya Allaah iwe juu yenu.”

na akiugeuza uso wake kiasi fulani upande wa kulia[4].

Wakati wa kuleta Tasliym walikuwa wakiashiria kwa mikono yao upande wa kulia na upande wa kushoto. Akawaona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhiwa sallam) ambapo akasema:

“Ni kwa nini mnaashiria kwa mikono yetu kana kwamba ni mikia ya farasi ilio na wasiwasi? Anapoleta Tasliym mmoja wenu basi ageukie upande wa mwenzake na wala asiashirie kwa mkono wake.” Pindi baadaye waliposwali pamoja naye hawakufanya tena hivo. Katika upokezi mwingine imekuja:

“Inakutoshelezeni kuweka mikono yenu juu ya mapaja yenu kisha muwasalimieni ndugu zenu upande wa kulia na upande wa kushoto.”[5]

[1] Muslim (582), Abu Daawuud, an-Nasaa’iy na at-Tirmidhiy ambaye ameisahihisha.

[2] Abu Daawuud na Ibn Khuzaymah (2/87/1) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. ´Abdul-Haqq ameisahihisha katika ”al-Ahkaam” (2/56) vivyo hivyo an-Nawawiy na Haafidhw Ibn Hajar. Imepokelewa vilevile na ´Abdur-Razzaaq katika ”al-Muswannaf” (2/219), Abu Ya´laa katika ”al-Musnad” (3/1253), at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (2/67/3) na ”al-Mu´jam al-Awsatw” (2/2600/1) na ad-Daaraqutwniy kupitia njia nyingine.

[3] an-Nasaa’iy, Ahmad na as-Sarraaj kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[4] Ibn Khuzaymah, al-Bayhaqiy, adh-Dhwiyaa’ katika ”al-Mukhtaarah”, ´Abdul-Ghaniy al-Maqdisiy katika ”as-Sunan” (1/234) kwa cheni ya wapokezi Swahiyh, Ahmad na at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Awsatw” (2/32). al-Haakim ameisahihisha adh-Dhahabiy na Ibn-ul-Mulaqqin wakaafikiana naye. Imetajwa katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (327).

[5] Muslim, Abu ´Awaanah, as-Sarraaj, Ibn Khuzaymah na at-Twabaraaniy.

Tanbihi!

Ibaadhiyyah wameipotosha Hadiyth hii. Rabiy´ wao ameipokea katika “al-Musnad” yake isiyojulikana kwa tamko lingine ili kutumia hoja kwamba kunyanyua mikono wakati wa kuleta Takbiyr ndani ya swalah ni jambo linalobatilisha swalah, kama wanavosema. Mmoja wao ni as-Sayyaabiy ambaye ameraddiwa katika utangulizi. Tamko lao ni la batili na ubainifu wake unapatikana katika ”adh-Dhwa´iyfah” (6044).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 163-164
  • Imechapishwa: 14/01/2019