107. Shahidi aliyekufa kwa maradhi ya tumbo

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuna aina tano ya mashahidi; mwenye kufa kwa tauni, mwenye kufa kwa maradhi ya tumbo, mwenye kuzama, mwenye kufa kwa kuangukiwa na jengo na shahidi katika njia ya Allaah.”

´Allaamah Ismaa´iyl at-Taymiy al-Aswbahaaniy amesema pindi alipokuwa akiifasiri Hadiyth:

“Maradhi ya tumbo ni yule mwenye kupatwa na maradhi tumboni.”

Wanachuoni wengine wamefasiri maradhi ya tumbo kwa njia tatu:

1- Mwenye kufa kwa maji kujaa tumboni (ascites).

2- Mwenye kufa kwa kutokupata choo.

3- Mwenye kufa kwa kuharisha.

Tafsiri ya tatu ndio yenye nguvu kwa mujibu wa wanachuoni wengi. Baadhi ya wanachuoni hawakutaja kitu kingine. Kuna uwezekano vilevile kwamba kufa shahidi kunahusu maradhi yote matatu – na Allaah ndiye anajua zaidi. Ni jambo linaloendana bora zaidi na ukarimu na kuenea kwa fadhila za Allaah. Kinachotilia nguvu hilo ni Hadiyth iliyopokelewa na Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Salmaan bin Muraad na Khaalid bin ´Arafah aliyeeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufa kwa sababu ya tumbo lake hatoadhibiwa ndani ya kaburi lake.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 227
  • Imechapishwa: 18/12/2016