107. Da´wah yetu ni yenye kupambanua baina ya haki na batili

Ni wajibu kwa vijana wa Kiislamu kuzindukana juu ya jambo hili na wala wasidanganyike na madai yenye kupotosha na kwamba eti yeyote anayesema kuwa ni muislamu, basi huyo ni muislamu. Haijalishi kitu japokuwa atafanya kitenguzi cha Uislamu. Sisi hatufarikishi watu. Tunachotaka ni kutenganisha kati ya mzuri na mbaya, mzuri na muovu. Amesema (Ta´ala):

قُل لَّا يَسْتَوِي الْخَبِيثُ وَالطَّيِّبُ وَلَوْ أَعْجَبَكَ كَثْرَةُ الْخَبِيثِ ۚ فَاتَّقُوا اللَّـهَ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ

”Sema: “Haviwi sawasawa vibaya na vizuri japokuwa utakupendekezea wingi wa vibaya. Basi mcheni Allaah, enyi wenye akili ili mpate kufaulu.” (al-Maaidah 05:100)

Sisi hatutenganishi kati ya waislamu. Sivyo kabisa. Tunatenganisha baina ya mzuri na muovu:

لِيَمِيزَ اللَّـهُ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ وَيَجْعَلَ الْخَبِيثَ بَعْضَهُ عَلَىٰ بَعْضٍ فَيَرْكُمَهُ جَمِيعًا فَيَجْعَلَهُ فِي جَهَنَّمَ ۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ

”Ili Allaah apambanue waovu na wema kisha aweke waovu juu ya waovu wengine, halafu awarundike pamoja awatie katika Moto wa Jahannam – hao ndio waliokhasirika.” (al-Anfaal 08:37)

Allaah katenganisha kati ya mbaya na mzuri. Yule asiyetanganisha baina ya mzuri na mbaya huyu ima hana akili ya kupambanua au hana imani kabisa. Kwa mujibu wake anawaona watu wote ni sawasawa. Hana imani inayomfanya kupambanua kati ya muumini na mnafiki, kafiri na muislamu, mkanamungu na zandiki. Hana kupambanua kati ya watu. Huyu ima ni punguani wa akili  au ´Aqiydah yake ni mbovu. Kwa hivyo ni wajibu kwa muislamu ayajue mambo haya na azingatie Aayah hii:

أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ

“Sema:  Je, mlikuwa mnamfanyia istihizai Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?” Hivyo msitoe udhuru, kwani mmekwishakufuru baada ya kuamini kwenu.” (at-Tawbah 09:65-66)

Mwenye kufanya mzaha Allaah na Mtume wake udhuru wake haukubaliki. Kuna dalili vilevile yenye kuonyesha kuwa mwenye kumtukana Allaah na Mtume wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anakufuru.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 137-138
  • Imechapishwa: 25/12/2018