106. Ihsaan, aina zake na nguzo yake


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Ngazi ya pili: Ni Ihsaan. Ina nguzo moja, nayo ni “kumwabudu Allaah kama vile unamuona. Ikiwa wewe humuoni, basi Yeye Anakuona”.

MAELEZO

Maana ya Ihsaan katika lugha ni kukifanya vizuri kitu na kukikamilisha. Ihsaan imegawanyika katika aina zifuatazo:

1-  Ihsaan kati ya mja na Mola Wake. Haya ndio malengo.

2- Ihsaan kati ya mja na watu wengine.

3- Ihsaan ya kiundwa na kukimairi. Mtu akiunda kitu au akafanya kazi fulani basi ni lazima kwake kuimairi na kuitimiza.

Aina ya kwanza ambayo ni Ihsaan kati ya mja na Mola Wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alibainisha jambo hilo  wakati ambapo Jibriyl alipomuuliza mbele ya Maswahabah, kama itavyokuja huko mbele, akasema:

“Ni kule kumwabudu Allaah kama vile unamuona. Ikiwa wewe humuoni, basi Yeye anakuona”.

Ihsaan kati ya mja na Mola Wake ni kuifanya vizuri kazi ambayo Allaah amemfaradhishia nayo kwa njia ya kwamba aifanye kwa njia ya sawa na kwa kumtakasia nia Allaah (´Azza wa Jall). Kitendo cha Ihsaan kati ya mja na Mola Wake ni kile kilichotimiza kumtakasia nia Allaah na pia kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alibainisha kuwa Ihsaan imegawanyika katika ngazi mbili:

Ya kwanza: Kumwabudu Allaah kama kwamba unamuona. Yakini ikufikishe kumwamini Allaah kama vile unamuona. Kwa msemo mwingine hauna mashaka wala kusita. Bali kama vile Allaah yuko mbele yako unamuona. Yule mwenye kufikia ngazi hii basi amefikia upeo wa mwisho wa Ihsaan. Unamwabudu Allaah kama vile unamuona kutokana na ukamilifu wa yakini na ukamilifu wa Ikhlaasw kama vile unamwona Allaah kwa macho. Allaah haonekani duniani bali ataonekana Aakhirah. Lakini unamuona kwa moyo wako kiasi cha kwamba ni kama vile unamuona kwa macho yako. Kwa ajili hiyo ndio maana watenda Ihsaan watalipwa kumuona (Subhaanahu wa Ta´ala). Wakati walipomwabudu kama vile wanamuona duniani ndipo Allaah akawalipa kwa kuwapa nafasi ya kumuona Yeye kwa macho yao katika makazi ya neema chungumzima. Amesema (Ta´ala):

لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ

“Kwa wale waliofanya wema watapata mazuri kabisa na ziada.”[1]

Ziada ni kumuona Allaah. Kwa sababu wao walifanya Ihsaan duniani ndipo Allaah akawapa Ihsaan ambayo ni Pepo na akawazidishia kumuona Allaah (´Azza wa Jall). Wamemwabudu Allaah kama vile wanamuona kwa macho, mapenzi na kutamani kukutana Naye. Vilevile wakapata ladha ya kumtii, wakapata utulivu wa kumtii na wakamtamani. Hii ndio hali ya watenda Ihsaan.

Ya pili: Ikiwa hukufikia ngazi hii kubwa basi mwabudu Allaah katika ngazi ya uchungaji. Hiyo ina maana kwamba ujue kuwa Allaah anakuona, anajua hali yako na anajua yaliyoko nafsini mwako. Kwa hiyo haikustahikii wewe kumwabudu, kwenda kinyume na amri Yake hali ya kuwa anakuona. Hii ni hali nzuri. Lakini iko chini kuliko ile ya kwanza. Midhali unajua kuwa anakuona basi ifanye vizuri ´ibaadah Yake na kuimairisha. Kwa sababu unatambua kuwa Allaah anakuona.

Allaah ni Mwenye sifa zilizo juu zaidi. Endapo ungelikuwa mbele ya kiumbe mwenye cheo fulani ambaye amekuamrisha amri fulani ambapo ukafanya amri hii mbele yake na yeye huku akutazama – je, inakustahikia kufanya upungufu katika kazi hiyo?

Kwa kufupiza ni kwamba Ihsaan ina ngazi mbili:

1- Ngazi ya kuona kwa moyo. Ni kule kumwabudu Allaah kama vile unamuona kutokana na yakini na imani yako yenye nguvu kiasi cha kwamba ni kama kwamba unamuona Allaah (´Azza wa Jall).

2- Ngazi hii iko chini kuliko ya kwanza. Ni wewe kumwabudu Allaah na huku unajua kuwa anakuona na anajua hali yako. Hivyo usimwasi na wala usende kinyume na amri Yake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Hizi ndio ngazi za Ihsaan na ndio ngazi za dini zilizo juu zaidi. Yule mwenye kuzifikia basi amefikia ngazi za dini zilizo juu zaidi, kabla yake kuna ngazi ya imani na kabla yake kuna ngazi ya Uislamu.

Dini inazunguka katika mizunguko ifuatayo:

Wa kwanza: Uislamu. Ni mpana kiasi cha kwamba ndani yake anaingia mpaka mnafiki. Anaitwa muislamu na anataamiliwa kama waislamu wengine. Kwa sababu amejisalimisha kwa uinje. Kwa hiyo ni mwenye kuingia katika mzunguko wa Uislamu. Vilevile anaingia yule muislamu mwenye imani dhaifu ambaye imani yake ni sawa na mbegu ya hardali.

Wa pili: Imani. Ni nyembamba zaidi kuliko wa kwanza. Ni mzunguko wa imani. Ndani yake haingii kabisa mnafiki mwenye unafiki wa uliofungamana na ´Aqiydah. Ndani yake wanaingia waumini ambao wamegawanyika aina mbili: wenye imani kamilifu na wenye imani pungufu. Anaingia ndani yake muumini mtenda madhambi na muumini mchaji.

Wa tatu: Ni nyembamba zaidi kuliko wa pili. Ni mzunguko wa Ihsaan. Ni kama alivyobainisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hawaingii ndani yake isipokuwa wale waumini wenye imani kamilifu.

[1] 10:26

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 221-225
  • Imechapishwa: 27/01/2021