103. Asiyeamini ngazi hizi za Qadar anazingatiwa hakuamini Qadar

Imani ya kuamini Qadar ndani yake kuna ngazi nne. Yule asiyeziamini zote basi anazingatiwa sio mwenye kuamini Qadar:

Ya kwanza: Elimu. Kuamini kwamba Allaah alikijua kila kitu milele. Alijua kila kitachopitika; yaliyokuweko na yatayokuweko pasi na mwisho. Allaah alijua milele kabla hayajakuwa na kabla hayajatokea. Alijua (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa elimu Yake ya milele ambayo anasifika nayo milele na siku zote. Hii ndio ngazi ya elimu. Mwenye kupinga ngazi hii ni kafiri.

Ya pili: Uandishi katika ubao uliohifadhiwa. Allaah alikiandika kila kitu katika ubao uliohifadhiwa. Hakupitiki kitu isipokuwa kimeandikwa katika ubao uliohifadhiwa. Hakuna kinachopitika ambacho hakikuandikwa. Kwa ajili hii amesema (Ta´ala):

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa upo katika Kitabu, kabla hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.”[1]

Bi maana ubao uliohifadhiwa. Allaah ndani yake ameandika makadirio ya kila kitu. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kitu cha kwanza alichoumba Allaah ni kalamu. Akaiambia: “Andika.” Ikasema: “Niandike nini?” Akasema: “Andika kila kitachokuwa mpaka kisimame Qiyaamah.”[2]

Yule mwenye kupinga uandishi na akasema kuwa Allaah anajua kila kitu lakini hata hivyo hakukiandika chochote katika ubao uliohifadhiwa ni kafiri na ni mwenye kuritadi nje ya dini ya Uislamu.

Ya tatu: Matakwa ya Allaah yenye kutendeka. Allaah hukitaka kitu. Hakuna kitu kinachotokea isipokuwa Allaah amekitaka kama ilivyoandikwa kwenye ubao uliohifadhiwa na kama alivyojua (Subhaanahu wa Ta´ala). Anakitaka kila kitu ndani ya wakati wake kinapozuka. Hakuzuki kitu pasi na kutaka kwa Allaah. Mwenye kusema kuwa mambo hutokea bila Allaah kuyataka ni kafiri.

Ya nane: Uumbaji. Allaah ndiye muumbaji wa kila kitu. Allaah akikitaka basi anakiumba. Kila kitu kimeumbwa na Allaah na ni katika uumbaji Wake na wakati huohuo ni kitendo na chumo la waja.

Ni lazima kwa mtu kuamini ngazi hizi nne. Vinginevyo mtu anazingatiwa sio mwenye kuamini Qadar: ngazi ya elimu, uandishi, utashi na uumbaji. Zote hizi ni lazima kuziamini. Mwenye kupinga chochote katika hayo basi ni murtadi na ni mwenye kutoka nje ya Uislamu. Kwa sababu amepinga nguzo miongoni mwa nguzo za imani ambayo ni kuamini Qadar.

[1] 57:22

[2][2] Abu Daawuud (4700) na at-Tirmidhiy (2155).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 217-219
  • Imechapishwa: 26/01/2021