102. Nguzo ya kuamini siku ya Mwisho na kuamini Qadar

5- Siku ya Mwisho: Imani ya kuamini siku ya Mwisho ni nguzo ya tano. Makusudio ya siku ya Mwisho ni siku ya Qiyaamah. Imeitwa “siku ya Mwisho” kwa sababu ni baada ya siku ya kwanza ambayo ni duniani. Dunia ni siku ya kwanza. Qiyaamah ndio siku ya Mwisho. Imani ya kuamini siku ya Mwisho inahusiana na imani ya kuamini yanayokuja baada ya kufa katika adhabu na neema za ndani ya kaburi, maswali ya Malaika wawili ndani ya kaburi. Kila kitachopitika ndani ya kaburi ni imani ya kuamini siku ya Mwisho. Vivyo hivyo kuamini kufufuliwa, kukusanywa, hesabu, kupimwa kwa matendo, njia, mizani ambayo itayapima matendo mema na maovu, Pepo na Moto. Upambanuzi wa yatayopitika siku ya Mwisho tunayaamini kwa njia ya jumla na kwa njia ya upambanuzi kwa kuanzia kifo mpaka pale ambapo watu wa Peponi watatulizana Peponi na watu wa Motoni Motoni. Kila kilichosihi katika mambo haya tunakiamini na wala hatutilii shaka kwa chochote katika hayo. Yule mwenye kutilia shaka chochote katika hayo ni kafiri na ameritadi nje ya Uislamu. Yote haya na yaliyomo ndani yake yanaitwa kuwa ni siku ya Mwisho.

6- Kuamini Qadar kheri na shari zake: Mtu anatakiwa kuamini kwamba yanayopitika katika ulimwengu huu katika kheri na shari, kufuru na imani, neema na majanga, raha na shida, maradhi na afya njema, uhai na kufa na mengine yote yanayopitika katika ulimwengu huu yamekadiriwa na si kwamba yametokea kwa bahati nasibu au kwamba yametokea hivihivi na hayakutanguliwa na Qadar. Mtu anatakiwa kuyaamini yote haya kwamba yametokea kwa mipango na makadirio ya Allaah. Vilevile mtu anatakiwa kuamini kwamba yaliyompata mtu hayakuwa ya kumkosa na yaliyomkosa hayakuwa ya kumpata na kwamba haya yametokea kwa mipango na makadirio ya Allaah. Amesema (Ta´ala):

مَا أَصَابَ مِن مُّصِيبَةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا فِي أَنفُسِكُمْ إِلَّا فِي كِتَابٍ مِّن قَبْلِ أَن نَّبْرَأَهَا ۚ إِنَّ ذَٰلِكَ عَلَى اللَّـهِ يَسِيرٌ

“Hausibu msiba wowote katika ardhi au katika nafsi zenu isipokuwa upo katika Kitabu, kabla hatujautokezesha. Hakika hayo kwa Allaah ni mepesi.”[1]

Hii ndio maana ya kuamini Qadar.

[1] 57:22

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 215-217
  • Imechapishwa: 25/01/2021