102. al-Qummiy upotoshaji wake wa kumi na mbili wa an-Nisaa´


al-Qummiy amesema wakati alipokuwa akifasiri Aayah:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا ثُمَّ آمَنُوا ثُمَّ كَفَرُوا ثُمَّ ازْدَادُوا كُفْرًا لَّمْ يَكُنِ اللَّـهُ لِيَغْفِرَ لَهُمْ وَلَا لِيَهْدِيَهُمْ سَبِيلًا

“Hakika wale walioamini kisha wakakufuru halafu wakaamini kisha wakakufuru, kisha wakazidi kufuru, Allaah hatowasamehe na wala hatowaongoa njia.”[1]

“Imeteremka juu ya wale waliomuamini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kumtambua bila ya kumsadikisha. Baada ya hapo wakakufuru pale walipoandika mkataba wa ndani kuhusu kwamba kamwe wasiache uongozi uwe katika watu wa familia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wakati Suurah “al-Wilaayah” ilipoteremka na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akachukua ahadi kutoka kwao juu ya kwamba kiongozi wa waumini ndiye anatakiwa kushika uongozi baada yake, wakaamini kwa kujifanya wamekubali bila ya kusadikisha. Pindi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipofariki wakakufuru na wakazidi kufuru.”[2]

Allaah akupige vita! Ni ujasiri ulioje ulionao wa kumzulia uongo Allaah na Mtume Wake! Ni ujasiri ulioje ulionao wa kukikengeusha Kitabu cha Allaah na kuwakufurisha watu bora kabisa baada ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam)!

Ni tarehe ngapi kuliandikwa mkataba huu? Ni lini kulipitika makubaliano haya ya siri ambayo hakuna awezaye kuyafanya isipokuwa Baatwiniyyah mfano wenu ambao kiu chao kikubwa ni kutafuta mambo ya kidunia, uongozi na fitina? Jambo ni la khatari kwa sababu nyinyi mnafikiri kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakutumwa kwa jengine isipokuwa tu kukita uongozi wa milele kwa watu familia yake.

Mnapotosha ujumbe wenye kuenea wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambao uko na uvumilivu, huruma kwa walimwengu, kuipa kisogo dunia, uchaji, ukweli na tabia za hali ya juu na kuupeleka katika lengo lisilotofautiana na wale wanaotafuta mambo ya kidunia na uongozi. Mmewaahidi wao na nyinyi dunia na Aakhirah kwa kutumia jina la familia ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kumzulia uongo Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Kitabu Chake bali na watu wa familia yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hawakuwalingania watu ufalme huu, uongozi na utumwa huu.

Ni lini kuliandikwa mkataba huu ambao Qur-aan imeteremshwa kwa ajili yake na amba kwa ajili yake wamekufurishwa Maswahabah? Uongo huu ni katika Wahy wa shaytwaan. Uongo huu ni katika matusi makubwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Uislamu na Qur-aan.

[1] 04:137

[2] Tafsiyr al-Qummiy (1/156).

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intisaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 150-151
  • Imechapishwa: 10/01/2018