101. Tafsiri ya Aayah “Nitakapomsawazisha na nikampuliza kitu katika roho Yangu”

Mwenye kutumia dalili ya kwamba roho imeegemezwa kwa Allaah (Ta´ala) katika maneno Yake:

فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ

“Nitakapomsawazisha na nikampuliza kitu katika roho Yangu, basi muangukieni kumsujudia.” 15:29

anatakiwa kutambua kuwa vitu vinavyoegemezwa kwa Allaah viko sampuli mbili:

1- Sifa zisizoweza kuwa peke yake kama mfano wa ujuu, uwezo, maneno, usikizi na uoni. Katika hali hii ni kuziegemeza sifa kwa Allaah mwenye kusifika nazo. Sifa za Allaah hazikuumbwa. Kadhalika inahusiana na uso na mkono Wake (Subhaanahu wa Ta´ala).

2- Kitu kinachoweza kuwa peke yake kuegemezwa kwa Allaah, kama mfano nyumba ya Allaah, ngamia wa Allaah, mja wa Allaah, Mtume wa Allaah na roho ya Allaah. Maneno haya yanayoegemezwa kwa Allaah yameumbwa na kuundwa na Allaah. Katika hali hii kile kilichoegemezwa kinakuwa na umaalum na utukufu ili kiweze kuwa tofauti na vyengine. Mfano wa hilo ni kama nyumba ya Allaah ingawa nyumba zote ni za Allaah. Kadhalika ngamia wa Allaah ingawa ngamia wote ni viumbe wa Allaah. Vitu vyote hivi kuegemezwa kwa Allaah ni ishara ya kwamba anavipenda na kuvitukuza. Na tofauti na pindi vitu kwa jumla vinapoegemezwa kwa Mola. Katika hali hii kunaashiriwa kwamba Yeye ndiye kaviumba na kufanya vipatikane. Kwa hiyo pindi vitu kwa jumla vinapoegemezwa kwa Allaah, kunaashiria kuwa Yeye ndiye kaviumba, na pindi vitu maalum vinapoegemezwa kwa Allaah, kunaashiria kuwa Ameviteua. Allaah anaumba na kuchagua anachotaka. Pindi roho inapoegemezwa kwa Allaah kunaashiria sampuli hii maalum na si ile ya jumla. Zingatia haya. Yatakufaa kutokamana na kutotumbukia kwenye Bid´ah. Watu wengi wamepinda katika suala hili. Tunamuomba Allaah kinga.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Muhammad al-Hanbaliy al-Manbajiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tasliyatu Ahl-il-Maswaa-ib, uk. 218-219
  • Imechapishwa: 12/12/2016