101. Kusherehekea mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)

Ni kujifananisha na wakristo katika kitendo kinachoitwa “kusherehekea mazazi ya al-Masiyh”. Waislamu wajinga au wanazuoni wenye kupotosha watu wanasherehekea katika Rabiy´ al-Awwaal au wakati mwingine kila mwaka kwa mnasaba wa kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wako ambao wanasherehekea sherehe hizi misikitini, wengine wanasherehekea majumbani au sehemu zilizoandaliwa kwa ajili ya jambo hilo na zinahudhuriwa na watu wengi katika watu ambao ni duni na wale wasiokuwa na elimu. Wanafanya hayo kwa kujifananisha na wakristo juu ya uzushi wao wa kusherehekea mazazi ya al-Masiyh (´alayhis-Salaam).

Mara nyingi sherehe hizi – licha ya kwamba ni uzushi na ni kujifananisha na wakristo – hazisalimiki na shirki na mambo maovu. Kama mfano wa kuimba mashairi ambayo ndani yake kuna kuchupa mpaka juu ya haki ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenda katika daraja kumuomba yeye badala ya Allaah na kumtaka msaada. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kuvuka mpaka wakati wa kumsifu pale aliposema:

“Msinisifu kwa kupitiliza kama walivyomsifu kwa kupitiliza ´Iysaa, mwana wa Maryam. Hakika mimi si vyenginevyo ni mja. Hivyo basi, semeni “Mja na Mtume Wake.”[1]

Sherehe hizi wakati mwingine zinakuwa na mchanganyiko kati ya wanaume na wanawake, uharibifu wa tabia, kudhihiri vilevi na mengineyo. Wakati mwingine wanaamini kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anahudhuria sherehe zao.

Miongoni mwa maovu yanayoandamwa na sherehe hizi ni Anaashiyd za pamoja zinazotumbwizwa, kupiga ngoma na mengineyo katika matendo ya Adhkaar za Suufiyyah zilizozuliwa. Pengine zikawa na mchanganyiko kati ya wanaume na wanawake, jambo ambalo husababisha fitina na linapelekea kutumbukia katika machafu. Haijalishi kitu hata kama sherehe hizi zitasalimika kutokamana na makatazo haya na wakaishilia tu kukusanya, kubadilishana vyakula na kudhihirisha furaha – kama wanavosema – itambulike kuwa ni Bid´ah iliyozuliwa:

“Kila kitachozuliwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”[2]

Isitoshe ni njia inayopelekea kuyakuza na kutokea maovu yanayotokea katika sherehe nyenginezo.

Tumesema kuwa ni Bid´ah kwa sababu haya msingi wowote katika Qur-aan, Sunnah, matendo ya as-Salaf as-Swaalih na karne bora. Yamezuliwa nyuma baada ya karne ya nne ya Hijriy. Walioyazua ni Faatwimiyyuun ambao ni Shiy´ah. Imaam Abu Hafsw Taaj-ud-Diyn al-Faakihaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

“Amma ba´d: Limekariri swali la kundi la wale wenye kutafuta baraka kwa kukusanyika ambako kunafanywa na baadhi ya watu katika mwezi wa Rabiy´ al-Awwaal na wanaita kuwa ni ´maulidi` na wanauliza kama yana msingi wowote katika dini? Wamekusudia nijibu hilo na kuwawekea wazi kwa ubainifu. Nikasema baada ya kumuomba Allaah tawfiyq:

“Sijui kuwa maulidi haya yana msingi wowote katika Qur-aan wala Sunnah. Hayakunakiliwa kutoka kwa yeyote katika wanachuoni wa Ummah ambao ndio kiiigizo chema katika dini na wenye kushikamana barabara na mapokezi ya wale waliotangulia. Bali ni Bid´ah iliyozuliwa na watu wasiokuwa na kazi na watu wenye matamanio ya nafsi ambao kazi yao ni kula.”[3]

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

“Vivyo hivyo yale yaliyozuliwa na baadhi ya watu ima kwa ajili ya kujifananisha na wakristo juu ya kuzaliwa kwa ´Iysaa (´alayhis-Salaam) au kwa ajili ya kumpenda na kumtukuza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)… katika kufanya mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuwa ni sikukuu pamoja na kwamba watu wametofautiana juu ya kuzaliwa kwake. Hakika kitendo hichi hakikufanywa na Salaf. Lau kitendo hichi kingelikuwa ni kheri tupu au kheri yenye nguvu zaidi basi Salaf (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa na haki zaidi [ya kuyafanya] kuliko sisi. Kwani hakika wao walikuwa wakimpenda Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakimtukuza zaidi kuliko sisi. Isitoshe wao ni wenye pupa zaidi juu ya kheri. Si vyenginevyo kumpenda na kumtukuza ni kwa kumfuata, kumtii, kufuata amri yake na kuhuisha Sunnah zake kwa uinje na kwa undani, kueneza yale aliyotumilizwa nayo, kupambana juu ya hayo kwa moyo, mikono na mdomo. Huu ndio mwenendo wa wale waliotangulia wa mwanzo katika Muhaajiruun, Answaar na wale waliowafuata kwa wema.”[4]

Kumeandikwa vitabu na vijitabu kwa ajili ya kukemea Bid´ah hapo kale na hivi sasa. Pamoja na kwamba ni Bid´ah na ni kujifananisha ni jambo ambalo vilevile linapelekea kusherehekea maulidi mengine kama mfano wa maulidi ya mawalii, ya Mashaykh na viongozi wao. Kwa hivyo yanafungua milango mingi ya shirki.

[1] al-Bukhaariy (3445).

[2] Ahmad (17184), Abu Daawuud (4607) na tamko ni lake, at-Tirmidhiy (2681) na Ibn Maajah (42).

[3] Risaalat-ul-Mawlid fiy ´amal-il-Mawlid, uk. 20-21.

[4] Iqtidhwaa´-us-Swiraatw al-Mustaqiym (02/615) kwa uhakiki wa Dr. Naaswir al-´Aqil.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Aqiydat-ut-Tawhiyd, uk. 193-196
  • Imechapishwa: 09/07/2020