101. al-Qummiy upotoshaji wake wa kumi na moja wa an-Nisaa´


al-Qummiy amesema wakati alipokuwa akifasiri Aayah:

إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ ۚ قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا ۚ فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Hakika wale waliyofishwa na Malaika hali ya kuwa wamejidhulumu nafsi zao [wataulizwa]: “Mlikuwa katika hali gani?”  Watasema: “Tulikuwa wadhaifu na wenye kukandamizwa katika ardhi”, watasema: “Je, hivi ardhi ya Allaah haikuwa pana mkahama ndani yake?” Basi hao makazi yao yatakuwa ni Motoni – na uovu ulioje mahali pa kuishia!”[1]

“Imeteremshwa juu ya wale waliompa mgongo kiongozi wa waumini na hawakupigana bega kwa bega wakiwa pamoja naye. Malaika watawauliza wakati wa kufa:

فِيمَ كُنتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ

“Mlikuwa katika hali gani?”  Watasema: “Tulikuwa wadhaifu na wenye kukandamizwa katika ardhi.”

Bi maana hatukuwa tunajua ni nani aliye na haki.  Ndipo Allaah akasema:

أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا

“Je, hivi ardhi ya Allaah haikuwa pana mkahama ndani yake?”

Bi maana dini ya Allaah na Kitabu Chake ni vipana mngeliweza kutafiti:

فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Basi hao makazi yao yatakuwa ni Motoni – na uovu ulioje mahali pa kuishia!”[2]

1- Kutakasika ni kwa Allaah kutokamana na mapungufu! Baatwiniyyah hawa wanajifanya kumsahau Allaah, Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Uislamu na wanakifungamanisha kila kitu kwa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesema:

“Mimi si vyenginevyo ni mtu wa kawaida katika waislamu.”

2- Sababu ya Aayah ni yenye kutambulika kwa wanachuoni na wafasiri wa Qur-aan, si hawa waongo wanaokipotosha Kitabu cha Allaah. al-Bukhaariy amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Ibn ´Abbaas aliyesema katika zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuna waislamu waliokuwa wakiishi pamoja na washirikina na wakiiongeza idadi ya washirikina. Ikatokea wakapatwa na mishale na wakafa au ikawapata shingoni mwao ndipo Allaah akawa ameteremsha Aayah[3]. Maneno ya mwongo huyu ya kwamba Aayah imeteremshwa juu ya wale walioacha kupigana bega kwa bega pamoja na ´Aliy ni aina ya uongo mbaya kabisa.

3- Vita kati ya ´Aliy na wapinzani wake haikuwa jambo ambalo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilipendekeza. ´Aliy aliulizwa kama kuna kitu alichosema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya vita hivi ambapo akajibu kwa kusema:

“Hapana.”

Bali uhakika wa mambo ni kwamba kumekuja Hadiyth Swahiyh zinazotahadharisha juu ya hilo. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kutakuwa na fitina. Yule mwenye kukaa katika [fitina] hizo ni bora kuliko yule mwenye kusimama, yule mwenye kusimama katika [fitina] hizo ni bora kuliko yule mwenye kutembea, yule mwenye kutembea katika [fitina] hizo ni bora kuliko yule mwenye kukimbia. Yule mwenye kuziingia zitamfanya vibaya na yule mwenye kuweza kupata upenyo wa kukimbia basi na afanye hivo.”[4]

“Pindi watakabiliana waislamu wawili kwa silaha zao basi muuaji na muuliwaji wote wawili wataingia Motoni.”[5]

Wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amesimama na akikhutubu akaja mjukuu  wake al-Hasan (Radhiya Allaahu ´anh) ambapo akawa amesema:

“Mtoto wangu huyu ni bwana. Huenda Allaah akasuluhisha kupitia yeye kati ya makundi mawili ya kiislamu makubwa.”[6]

Haya yanathibitisha kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakufurahishwa na vita hivi. Kwa ajili hiyo ndio maana Maswahabah wengi waheshimiwa na wanachuoni walijiepusha navyo. Kama mfano wa Sa´d bin Abiy Waqqaas, Muhammad bin Maslamah, ´Abdullaah bin ´Umar na Usaamah bin Zayd. Hakuna yeyote aliyewakandamiza. Walikuwa na nafasi ya juu katika Ummah wa Kiislamu. Kwa sababu hiyo ndio maana al-Hasan hakupigana. Wakati alipopata uongozi akamwachia nao Mu´aawiyah na kwa ajili hiyo yakathibiti kwake maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Huenda Allaah akasuluhisha kupitia yeye kati ya makundi mawili ya kiislamu makubwa.”

Ummah wa Kiislamu ukamshukuru sana kwa hilo kwa sababu ya kupatikana kheri kubwa kama vile umoja wa waislamu, kulindwa damu zao na Jihaad katika njia ya Allaah ili kulinyanyua neno la Allaah. Ni dhambi kubwa ilioje aliyotumbukia ndani yake Baatwiniy huyu pale anaposema:

“Imeteremshwa juu ya wale waliompa mgongo kiongozi wa waumini na hawakupigana bega kwa bega wakiwa pamoja naye.”!

Dhambi kubwa zaidi kuliko hiyo ni pale aliposema:

“Malaika watawauliza wakati wa kufa:

فِيمَ كُنتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ

“Mlikuwa katika hali gani?”  Watasema: “Tulikuwa wadhaifu na wenye kukandamizwa katika ardhi.”

Bi maana hatukuwa tunajua ni nani aliye na haki. “

Hivi kuna ujasiri mbaya wa kukipotosha Kitabu cha Allaah kuliko huu? Kuna uongo mkubwa kumzulia Allaah na Malaika kuliko huu?

Je, Aayah hii imeteremshwa katika vita vya ngamia na vita vya Swiffiyn?

Je, muongo huyu aliwaona Malaika wakiwateremkia wale wote walioacha kupigana bega kwa bega pamoja na ´Aliy wakati wa kufa?

Je, alimsikia Allaah akisema:

أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا

“Je, hivi ardhi ya Allaah haikuwa pana mkahama ndani yake?”

na alijua kuwa Allaah anakusudia kwamba dini Yake ni pana na wangeliweza kutafiti ndani Yake? Si jengine isipokuwa ni uongo wa Baatwiniyyah na ukiukaji wa Kitabu cha Allaah na kumchezea shere:

قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ

“Je, mlikuwa mnamfanyia mzaha Allaah na Aayah Zake na Mtume Wake?”[7]

[1] 04:97

[2] Tafsiyr al-Qummiy (1/149).

[3] 4596.

[4] al-Bukhaariy (7081) na Muslim (2886).

[5] al-Bukhaariy (31) na Muslim (2888).

[6] al-Bukhaariy (2704).

[7] 09:65

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Intisaar li Kitaab-il-´Aziyz al-Jabbaar, uk. 148-150
  • Imechapishwa: 10/01/2018