100. Anapinga uwepo wa Malaika au analeta tafsiri za kipotofu


Imani ya kuamini Malaika ni nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu. Yule mwenye kuwapinga Malaika na akasema kuwa hakuna Malaika kwa sababu hatuwaoni anakuwa ni kafiri, mkanamungu na zandiki. Kwa sababu mtu huyu haamini mambo yaliyofichikana.

Vivyo hivyo inahusiana na yule ambaye anapindisha na kusema kuwa Malaika ni maana tu na sio viwiliwili na kwamba ni zile hisia zinazomjia mtu. Hisia hizo zikiwa nzuri basi huyo ni Malaika na hisia hizo zikiwa mbaya basi huyo n shaytwaan. Haya ni maneno ya kikafiri. Kwa masikitiko makubwa yako katika “Tafsiyr-ul-Manaar” ambayo yamenukuliwa na Muhammad Rashiyd Ridhwaa kutoka kwa Shaykh wake Muhammad ´Abduh. Haya ni maneno ya wanafalsafa. Ni maneno batili. Mwenye kuyaamini ni kafiri. Lakini tunataraji kuwa aliyanukuu pasi na kuyaamini. Lakini kule kuyanakili bila kuyakosoa kuna khatari. Maneno haya ni batili na ni kuwakufuru Malaika. Tunamuomba Allaah afya na usalama.

Haitakiwi kwa mtu kuingiza akili na fikira zake au akanukuu kutoka kwa wanafalsafa au mazanadiki chochote katika mambo ya dini au mambo yaliyofichikana. Anachotakiwa ni kunakili kutoka katika Qur-aan na Sunnah, ndio jambo la wajibu.

Katika “Tafsiyr-ul-Manaar” imetajwa kwamba imenukuliwa kutoka katika “Ihyaa´ ´Uluum-id-Diyn” cha al-Ghazaaliy. Allaah ndiye anajua zaidi. Kitabu “Ihyaa´ ´Uluum-id-Diyn” cha al-Ghazaaliy ndani yake mna majanga na mabalaa ingawa ndani yake kuna kitu katika kheri na faida. Lakini ndani yake mna maangamizi na sumu kiwango kikubwa. Ni kitabu kilichochanganya mambo. Shari zake ni nyingi kuliko kheri zake. Kwa hivyo haipasi kwa yule mwanafunzi anayeanza au mtu wa kawaida kukisoma isipokuwa akiwa na elimu na uwezo wa kupambanua kati ya haki na batili.

Malaika sio maana kama wanavosema. Bali Malaika ni wenye viwiliwili na maumbo. Wana uwezo wa kujibadilisha kwa maumbo mbalimbali Allaah amewapa uwezo wa kufanya hivo. Kwa ajili hii Jibriyl (´alayhis-Salaam) alikuwa akimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika umbile la bwana mmoja. Allaah amewapa uwezo wa kuweza kujibadilisha katika maumbile mbalimbali kwa ajili ya manufaa ya mwanadamu. Kwa sababu mwanadamu hawezi kustahamili kuwaona Malaika katika umbile ambalo Allaah amewaumba kwalo. Walikuwa wanamjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika umbile la bwana mmoja kwa ajili ya kumfanyia urafiki mwanadamu. Hawaonekani katika umbile lao na uhakika wao isipokuwa wakati wa adhabu. Amesema (Ta´ala):

يَوْمَ يَرَوْنَ الْمَلَائِكَةَ لَا بُشْرَىٰ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُجْرِمِينَ

“Siku watakayowaona Malaika hakutakuwa na bishara njema Siku hiyo kwa wahalifu.”[1]

Vilevile wakati wa kifo mtu huwaona. Kipindi hicho humuona Malaika wa mauti. Lakini duniani na kipindi ambacho mtu bado anaishi hawaoni. Kwa sababu hana uwezo wa kuwaona.

Allaah amewaumba kutokana na nuru. Amewaumba mashaytwaan kutokana na moto, hivo ndivo ilivyotajwa katika Qur-aan. Amemuumba Aadam kutokana na udongo. Allaah juu ya kila jambo ni muweza.

Makafiri wanaamini kuwa Malaika ni wasichana wa Allaah. Amesema (Ta´ala):

وَجَعَلُوا الْمَلَائِكَةَ الَّذِينَ هُمْ عِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ إِنَاثًا ۚ أَشَهِدُوا خَلْقَهُمْ ۚ سَتُكْتَبُ شَهَادَتُهُمْ وَيُسْأَلُونَ

“Wakawafanya Malaika, ambao ni waja wa Mwingi wa huruma, kuwa ni wa kike. Je, kwani wameshuhudia uumbaji wao?  Hakika utaandikwa ushahidi wao na wataulizwa.”[2]

[1] 25:22

[2] 43:19

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Thalaathat-il-Usuwl, uk. 211-213
  • Imechapishwa: 25/01/2021