10. Vitu vyengine vyenye kuharibu swawm


Ee muislamu! Yatambue mambo mengine yanayoharibu swawm:

5- Kuumikwa

Damu inayoharibu swawm ni ile ya wakati wa kupiga chuku. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayefanya na anayefanyiwa chuku wametengua swawm.”[1]

Kipimo hukumu hiyo hiyo ina kila ambaye anakusudia kuitoa damu yake mwilini na ukadhoofika kwa udhaifu. Hilo linaharibu swawm kama kuumikwa. Upande mmoja Shari´ah ya Kiislamu haitofautishi baina ya vitu viwili vinavyofanana. Upande mwingine haikusanyi baina ya vitu viwili vinavyotofautiana.

Kuhusu ile damu inayomtoka mtu pasi na kukusudia, kama damu inayomtoka mtu puani, kujikata na kisu wakati wa kukata nyama au kukanyaga magaya, hayaharibu swawm. Katika hali hii haijalishi kitu hata kama mtu atapoteza damu nyingi. Hali kadhalika iwapo mtu atapoteza damu ndogo kama wakati wa vipimo. Haiathiri swawm.

6- Jimaa kwa kuingiza dhakari ndani ya tupu ya mwanamke

Mwanaume akimjamii mkewe mchana wa Ramadhaan ni wajibu kwa wote wawili kutoa kafara. Kafara ni kuachia mtumwa huru muumini. Wasipoweza basi ni juu yao kufunga miezi miwili mfululizo ikiwa mke alikubali kwa khiyari yake. Wasipoweza basi ni wajibu kwao kulisha masikini 60. Kila mmoja wao analazimika kutoa Swaa´ 30, ni takriban 90 kg, ya chakula kilichozoeleka katika mji kuwapa masikini 60. Kila masikini anatakiwa kupewa Swaa´ moja, takriban 3 kg, ambapo mwanaume atatoa nusu na mwanamke atatoa nusu. Haya ndio yanayowalazimu wasipoweza kuachia mtumwa huru na kufunga miezi miwili mfululizo. Isitoshe ni wajibu vilevile kulipa siku hiyo waliyofanya jimaa. Wanatakiwa pia watubu kwa Allaah, wajute, waache kitendo kama hicho na kumuomba Allaah msamaha. Kufanya jimaa mchana wa Ramadhaan ni dhambi kubwa. Asiwepo mwenye kufunga yeyote atayetumbukia katika kitendo kama hicho.

Hata hivyo iwapo mtu atakuwa safarini au akawa na maradhi yanayomruhusu kutofunga, hana juu yake kafara. Huyu hakufanya kosa lolote. Anachotakiwa tu ni kulipa siku hii ambayo alifanya jimaa. Kwa sababu inaruhusu kwa mgonjwa na msafiri kufanya jimaa na mengine wanapokuwa si wenye kufunga. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo.”[2]

Katika hili mwanamke ana hukumu moja kama mwanaume. Ikiwa swawm yake ni ya wajibu ni juu yake kutoa kafara na kulipa siku hiyo. Hata hivyo akiwa ni msafiri au mgonjwa ambaye swawm inamtia uzito, sio wajibu kwake kutoa kafara.

7- Kutoa manii kwa matamanio

Kutoa manii kwa matamanio kunatengua swawm. Ni mamoja ikiwa mtu amemwaga kwa sababu ya kujichua, kukisi, kuangalia kwa kukariri au kitu kingine kinachomfanya mtu kushukwa kama punyeto na kadhalika.

TANBIHI

Hapa yanafuata mambo yasiyoharibu swawm:

1- Wanja

Kwa mujibu wa maoni sahihi ya wanachuoni wanja hauharibu swawm ya mwanamke wala ya mwanaume. Lakini hata hivyo lililo bora kwa mfungaji autumie usiku. Hali kadhalika hukumu hiyo hiyo ina vipodozi vingine vyote kama sabuni, mafuta na vinginevyo vinavyopakwa mwilini. Mfano wa vitu hivyo ni hina, vipodozi na kadhalika. Ni sawa kwa mfungaji kutumia vyote hivyo. Lakini haifai kutumia vipodozi ikiwa vinaudhuru uso.

2- Dawa ya mswaki

Swawm haiharibiki kwa kuswaki kwa dawa ya mswaki. Ni kama Siwaak. Lakini mtu anatakiwa kuhakikisha hakumeza kitu katika dawa hiyo. Ikimteleza akameza kitu katika dawa sio wajibu kwake kulipa siku hiyo.

3- Dawa za matone ya macho na masikio

Dawa za matone ya macho na masikio haziharibu swawm kwa mujibu wa maoni sahihi ya wanachuoni. Ikiwa mtu atahisi ladha yake shingoni lililo salama zaidi ni kulipa siku hiyo. Lakini hata hivyo sio wajibu kwa sababu macho na masikio havina njia za kupitisha chakula na kinywaji.

Kuhusu dawa za matone ya pua hazijuzu kwa sababu kuna njia ya kupitisha chakula na kinywaji. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayh wia sallam) amesema:

“Yapandishe maji vizuri wakati wa kusukutua isipokuwa ikiwa kama utakuwa mfungaji.”[3]

Kujengea juu ya Hadiyth hii ni wajibu kwa mwenye kutumia dawa za matone ya pua kulipa siku hiyo.

4- Kuota na fikira za kimapenzi

Kuota na fikira za mapenzi haziharibu swawm hata kama zitamfanya mtu kumwaga. Mtu akiona manii ni wajibu kwake kuoga janaba. Akiota na kumwaga baada ya Fajr na akachelewesha mpaka Dhuhr hakuna neno. Hali kadhalika ikiwa atamwingilia mke wake usiku na akaoga baada ya kupambazuka alfajiri. Ni sawa. Imethibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anafanya jimaa usiku, anaamka asubuhi hali ya kuwa na janaba, akioga na kuendelea na swawm. Hali kadhalika mwenye hedhi na mwenye nifasi. Endapo watatwaharika usiku na wakaoga baada ya kuwa alfajiri imeshaingia hakuna neno na swawm zao ni sahihi. Lakini haijuzu kwa wanawake hawa, wala kwa yule aliye na janaba, kuchelewesha kuoga au swalah mpaka jua likachomoza. Bali ni wajibu kwao wote kuoga kabla ya jua kuchomoza ili waweze kuswali kwa wakati wake.

5- Kucheza na mke

Inafaa kwa mwanaume aliefunga kucheza na mke wake, kumbusu na kumkumbatia maadamu hawakufanya jimaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiwabusu na akiwakumbatia wakeze ilihali amefunga. Lakini mtu akichelea kutumbukia katika yale aliyoharamisha Allaah itakuwa yaliyotajwa ni haramu kwake. Endapo atamwaga anatakiwa kuendelea kufunga na ailipe siku hiyo. Hata hivyo kwa mujibu wa wanachuoni wengi hana juu yake kafara.

Kuhusu madhii, hayaharibu swawm kwa mujibu wa maoni sahihi ya wanachuoni. Asli ni kuwepo kwa swawm na madhii ni vigumu kuyaepuka.

6- Kumeza mate

Mate hayadhuru swawm kabisa. Ni sawa kumeza mate na ni sawa vilevile kuyatema.

Kuhusu makohozi yanayotoka kifuani au mapuani, ni wajibu kwa mwanaume na mwanamke kuyatema na asiyameze.

Ee waislamu! Swawm ni kitendo chema na kikubwa na thawabu zake ni tele na khaswa khaswa swawm ya Ramadhaan. Uadhimisheni – Allaah akurehemuni – kwa kuwa na nia njema na kujitahidi kuhifadhi swawm yake, kusimama nyusiku zake na kukimbilia matendo mema na kutubia madhambi na makosa yote. Tahadharini na yale Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) walokataza na mtiini katika Ramadhaan na wakati mwingine. Usianeni na saidianeni juu ya hayo. Amrisheni mema na katazeni maovu ili muweze kupata Pepo, furaha, utukufu na kufuzu duniani na Aakhirah.

Tunamuomba Allaah atuhifadhi sisi na nyinyi kutokamana na yale yote yenye kusababisha ghadhabu Zake, atukubalie swawm zetu na visimamo vyetu, azitengeneze hali za watawala wa waislamu na ainusuru dini Yake kupitia wao na awakoseshe nusura maadui Wake kupitia wao na awawafikishe wote waweze kuifahamu dini na kuwa na msimamo juu yake na kuhukumu na kuhukumiwa kwayo katika mambo yote. Hakika Yeye ni muweza juu ya hayo.

Swalah na salaam zimwendee mja na Mtume Wake, Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na wale wote wataofuata njia yake hadi siku hiyo ya Qiyaamah.

[1] Abu Daawuud (2367), at-Tirmidhiy (774), Ibn Maajah (1679) na Ahmad (15866). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (931).

[2] 02:185

[3] Abu Daawuud (2366), at-Tirmidhiy (788), an-Nasaa’iy (78), Ibn Maajah (407) na Ahmad (16430). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl” (930).