10. Upande


Kwa kichwa cha khabari hichi tunachotaka ni kubainisha kama upande umethibiti kwa Allaah (Ta´ala) au haukuthibiti. Uhakika wa mambo ni kwamba mtu hawezi kumthibitishia wala kumkanushia upande Allaah (Ta´ala) likitajwa pasi na kufungamanishwa. Katika hali hiyo swali ni lazima lifafanuliwe.

Ikiwa upande wa chini ndio makusudio, basi ni jambo lisilowezekana kwa Allaah. Bali haiwezekani kwa Allaah (Ta´ala) akasifika kwayo. Ni lazima Allaah (Ta´ala) asifike na ujuu kabisa kuhusiana na dhati na sifa Zake.

Ikiwa upande wa juu unaomfunika ndio makusudio, Allaah hasifiki nao. Bali ni jambo lisilowezekana kwa Allaah (Ta´ala) kusifika nao. Allaah ni Mkubwa na Mtukufu zaidi kufunikwa na kitu katika viumbe Wake. Itakuweje ilihali Kursiy yake imezunguka mbingu na ardhi?

وَالْأَرْضُ جَمِيعاً قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَى عَمَّا يُشْرِكُونَ

“Ataikamata ardhi yote siku ya Qiyaamah na mbingu zitakunjwa mkononi Mwake wa kuume.”[1]

Ikiwa makusudio ni upande wa juu wenye kulingana na ukubwa na utukufu Wake pasi na lengo la kumzunguka, hiyo ni haki na ndio imethibiti kwa Allaah (Ta´ala) na ni wajibu asifiwe nao. Shaykh Muhammad ´Abdul-Qaadir al-Jaylaaniy amesema katika kitabu chake “al-Ghunyah”:

“Yeye (Subhaanah) yuko katika upande wa juu. Amelingana juu ya ´Arshi na yuko na ufalme.”[2]

Ana ufalme maana yake ni kwamba (Tabaarak wa Ta´ala) anauzunguka.

Huenda mtu akauliza: Ni upi msimamo wenu juu ya yale ambayo Allaah amejithibitishia Mwenyewe katika Kitabu Chake, kupitia kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na waislamu wakaafikiana kwayo kuhusu kwamba Allaah (Subhaanah) yuko mbinguni?

Tunajibu kwa kusema Allaah kuwepo mbinguni, haina maana kuwa mbingu inamzunguka. Mwenye kusema hivo ni mpotevu na amesema hilo kutoka kichwani mwake. Akimnasibishia mwengine hili, atakuwa ima ni mwongo au mwenye kukosea. Hakika kila mwenye kutambua ukubwa wa Allaah (Ta´ala) na kukizunguka Kwake kila kitu na kwamba ardhi yote ataikamata siku ya Qiyaamah na kwamba atazikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu, hawezi hata siku moja kufikiria kuwa kitu katika viumbe kinaweza kumzunguka (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kujengea juu ya hili fiys-Samaa´ inaweza kuwa na maana mbili:

Ya kwanza: as-Samaa´ kuwa na maana ya ujuu. Katika hali hii itakuwa na maana kuwa Allaah yuko juu, bi maana upande wa juu. as-Samaa´ kuwa na maana ya juu ni jambo limethibiti katika Qur-aan. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُمْ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً

“Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni (as-Samaa´).”[3]

Bi maana kutoka juu na sio kutoka kwenye mbingu yenyewe kwa vile mvua inanyesha kutoka kwenye mawingu.

Ya pili: Kufanya fiy kuwa na maana yaa juu (´alaa). Katika hali hii itakuwa na maana kuwa Allaah yuko juu ya mbingu. Fiy imekuja kwa maana ya juu sehemu nyingi katika Qur-aan. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَسِيحُوا فِي الْأَرْضِ

“Basi tembeeni katika ardhi.”[4]

Bi maana juu ya ardhi.

[1] 39:67

[2] uk. 94

[3] 08:11

[4] 09:02

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fath Rabb-il-Bariyyah, uk. 38-39
  • Imechapishwa: 14/01/2020