10. Tawaaf-ul-Quduum [Twawaaf ya kufika]


27- Halafu mtu atafanya haraka kwenda katika jiwe jeusi, alielekee kisha aseme:

Imesihi kutoka kwa Ibn ´Umar kwamba alisema pia kabla yake:

الله أكبر

“Allaahu ni mkubwa.”

Amekosea yule aliyeiegemeza khabari hii kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye kafanya hivi.

28- Halafu ataligusa kwa mkono wake, kulibusu kwa mdomo wake na atasujudu juu yake vilevile. Hayo yamefanywa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ´Umar na Ibn ´Abbaas[1].

29- Isipomuwezekania yeye kulibusu, basi aliguse aliguse kwa mkono wake kisha aubusu mkono wake.

30- Isipomuwezekania yeye kuligusa, basi aliashirie kwa mkono wake.

31- Haya yanatakiwa kufanywa katika kila mzunguko.

32- Mtu hatakiwi kuleta msongamano juu yake. Alisema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Umar:

“Ee ´Umar! Hakika wewe ni mtu mwenye nguvu. Usimuudhi dhaifu. Ukitaka kuligusa jiwe, kusipokuwa watu liguse. Vinginevyo lielekee na useme “Allaahu Akbar.”[2]

33- Kuna fadhilah kubwa za kuligusa jiwe jeusi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ninaapa kwa Allaah kwamba Allaah atalifufua jiwe jeusi siku ya Qiyaamah. Litakuwa na macho mawili linaona kwa macho hayo na litakuwa na ulimi linazungumza kwa ulimi huo. Litamshuhudia yule aliyeligusa kwa haki.”[3]

Amesema tena:

“Kuligusa jiwe jeusi na nguzo ya upande wa yemeni, kunaporomosha madhambi kabisa.”[4]

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Jiwe jeusi linatokea Peponi. Lilikuwa jeupeee mno kuliko theluji kabla ya madhambi ya washirikina.”[5]

34- Kisha mtu aanze Twawaaf pembezoni mwa Ka´bah aifanye kushotoni kwake. Atatufe nje ya Hijr mizunguko saba. Kutoka kwenye kijiwe cheusi kimoja mpaka kwenye kijiwe cheusi tena ndio mzunguko mmoja. Anatakiwa kuvaa Ridaa´ yake na kuipitisha chini ya kwapa la kulia wakati wa Twawaaf yote. Katika mizunguko mitatu ya mwanzo, anatakiwa kwenda mbiombio. Kwenda mbiombio kunaaza na kuisha kwenye jiwe jeusi. Katika mizunguko mingine iliobaki anatakiwa kutembea.

35- Katika kila mzunguko atatakiwa kuigusa kona ya upande wa yemeni na wala asiibusu. Ipomuwezekania kuigusa, basi kuashiria kwa mkono ni jambo halikuwekwa katika Shari´ah.

36- Baina ya upande wa nguzo ya yemeni na jiwe jeusi mtu atasema:

ربنا آتنا في الدنيا حسنة وفي الآخرة حسنة وقنا عذاب النار

“Ee Mola wetu! Tupe duniani wema na Tupe Aakhirah wema na tukinge na adhabu ya Moto.”[6]

37- Wala hatozigusa zile nguzo mbili zilizoko upande wa Shaam kwa sababu ya kumuiga Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[7].

[1] Moja katika taaliki ya baadhi ya waheshimiwa katika ”al-Manaasik waz-Ziyaaraat”:

“Haya hayakupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

Huku ni kufikiria kwake tu. Nimepata kujua kuwa ni Swahiyh katika “al-Irwaa´” (1112) ambayo chapisho lake Allaah amelisahilisha – himdi na neema zote anastahiki Allaah.

[2] Ameipokea ash-Shaafi´iy, Ahmad na wengineo. Hadiyth ina nguvu, kama nilivyobainisha katika ”al-Haj al-Kabiyr”.

[3] Ameipokea at-Tirmidhiy, Ibn Khuzaymah, Ibn Hibbaan, al-Haakim na adh-Dhahabiy. Imetajwa katika marejeo yaliyotangulia.

[4] at-Tirmidhiy amesema ni nzuri wakati Ibn Hibbaan, al-Haakim na adh-Dhahabiy wamesema kuwa ni nzuri.

[5] Swahiyh kwa mujibu wa at-Tirmidhiy na Ibn Khuzaymah.

[6] Ameipokea Abu Daawuud na wengineo. Wengi wameonelea kuwa ni Swahiyh. Tazama ”Swahiyh Abiy Daawuud” (1653).

[7] Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

“Kuigusa bi maana kujipangusa kwa mkono. Ama sehemu iliyobaki ya Nyumba, sehemu ya Ibraahiym na misikiti mingine yote ya duniani na njia zake, makaburi ya Mitume na waja wema – kama mfano wa chumba cha Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na pango la Ibraahiym na mahali ambapo Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali ndani yake – na mwamba wa Yerusalemu, havitakiwi kuguswa wala kubusiwa. Haya ni kwa maafikiano ya maimamu. Kuhusu kufanya Twawaaf pembezoni mwa vitu hivi ni miongoni mwa Bid´ah kubwa kabisa zilizoharamishwa. Mwenye kuyachukulia mambo haya kama dini basi anatakiwa kuambiwa kutubia. Akitubia ni sawa. Vinginevyo auawe.

Ni uzuri ulioje wa yale aliyopokea ´Abdur-Razzaaq (8945), Ahmad na al-Bayhaqiy kutoka kwa Ya´laa bin Umayyah ambaye amesema:

“Nilifanya Twawaaf pamoja na ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) – katika upokezi mwingine pamoja na ´Uthmaan. Nilipofika kwenye kona inayotazamana na mlango ilio baada ya mlango, nilimshika mkono wake ili aiguse. Akasema: “Wewe hukufanya Twawaaf na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?” Nikasema: “Ndio.” Akasema: “Ulimuona akiligusa?” Nikasema: “Hapana.” Ndipo akasema: “Basi nenda! Kwani hakika wewe una kiigizo chema kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manaasik-ul-Hajj wal-´Umrah, uk. 20-22
  • Imechapishwa: 07/07/2018