10. Njia ya tatu: kumcha Allaah (´Azza wa Jall)

Miongoni mwa njia za kuipata elimu ni kumcha Allaah (´Azza wa Jall). Haina shaka kuwa kumcha Allaah ndio sababu ya kila kheri na matunda yake ni makubwa kwa mja. Vipi isiwe hivyo ilihali ndio wasia wa Allaah kwa wa mwanzo na wa mwisho?

وَلَقَدْ وَصَّيْنَا الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ وَإِيَّاكُمْ أَنِ اتَّقُوا اللَّـهَ

“Hakika Tumewausia wale waliopewa Kitabu kabla yenu na nanyi pia ya kwamba mumcheni Allaah.”[1]

Vilevile ndio wasia wa Allaah kwa Mitume wote. Kadhalika ndio wasia wa Allaah kwa watu wote. Pia ndio wasia wa Allaah kwa waumini wote. Vivyo hivyo ndio wasia wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa waumini. Hakika mara nyingi (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiusia kumcha Allaah. Vilevile ndio wasia wa wema waliotangulia. Hakika wema waliotangulia hawakuwa wakianza barua ya wasia kwa jengine isipokuwa wanaanza kwa kuusia kumcha Allaah. Kwa sababu kumcha Allaah (´Azza wa Jall) ni jambo limekusanya ndani yake kheri zote. Kumcha Allaah maana yake ni kumtii Allaah (´Azza wa Jall), juu ya nuru kutoka kwa Allaah na wakati huo huo ukitarajia thawabu za Allaah. Vilevile kuacha kumuasi Allaah, juu ya nuru ya Allaah kwa kuchelea isije kukupata adhabu ya Allaah. Kumcha Allaah kwa msemo mwingine ni Allaah akuone wewe kule alikokuamrisha na asikuone kule alikokukataza.

Kumcha Allaah (´Azza wa Jall) ni sababu ya kufikia elimu. Hili halina shaka yoyote. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ وَيُعَلِّمُكُمُ اللَّـهُ

“Mcheni Allaah na Allaah anakufunzeni.”[2]

Haina shaka kwamba kushikamana na mambo ya wajibu na kujiepusha na maasi ni sababu ya kuithibitisha elimu baada ya kuipata.

[1] 04:131

[2] 02:282

  • Mhusika: Shaykh Sulaymaan bin Saliymillaah ar-Ruhayliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-´Ilm wa Wasaaailuh wa Thimaaruh
  • Imechapishwa: 22/10/2016