10. Msingi wa tatu: Kumsikiliza na kumtii kiongozi

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Msingi wa tatu:

Miongoni mwa utimilifu wa umoja ni usikivu na utiifu kwa yule ambaye amekuwa kiongozi juu yetu hata kama atakuwa ni mtumwa wa kihabeshi. Allaah amebainisha haya ubainifu wenye kutosheleza kwa njia mbalimbali miongoni mwa aina za ubainifu Kishari´ah na kwa Qadar.

MAELEZO

Miongoni mwa utimilifu wa umoja…  – Msingi wa tatu ni kumtii mtawala wa waislamu. Kwa sababu umoja hautimii isipokuwa kwa kumtii mtawala. Hakuna mkusanyiko isipokuwa kwa kupatikana kiongozi na wala hakuna kiongozi isipokuwa kwa kuwepo usikivu na utiifu. Kiongozi wa waislamu Allaah amemfanya kuwa ni rehema kwa waislamu kwa kule kusimamisha adhabu za Kishari´ah, kuamrisha mema na kukataza maovu, kumnusuru mdhulumiwa kutokana na mdhulumaji, kudhibiti amani na mengineyo. Haya ni katika rehema za Allaah (´Azza wa Jall).

Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) alipokufa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hawakumzika isipokuwa mpaka baada ya kula kiapo cha usikivu kwa kiongozi wao. Hili ni kwa sababu wanachelea tofauti na fitina. Wanajua kuwa si sawa kuishi siku hata moja bila ya kuwa na kiongozi. Hili ni katika mambo ya lazima ya dini. Hakupatikani haya isipokuwa kwa kuwepo usikivu na utiifu kwa mtawala. Kwa ajili hii ndio maana Allaah (Jalla wa ´Alaa) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.” (04:59)

Baada ya kumtii Allaah na Mtume Wake ni lazima kumtii mtawala. Maneno Yake:

مِنكُمْ

“… katika nyinyi.”

bi maana katika waislamu. Ni dalili yenye kuonesha kuwa imeshurutishwa mtawala awe ni muislamu.

Allaah amebainisha haya ubainifu wenye kutosheleza kwa njia mbalimbali… – Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninakuusieni kumcha Allaah, kusikiliza na kutii hata kama mtatawaliwa na mtumwa. Hakika yule atakayeishi muda mrefu katika nyinyi basi ataona tofauti nyingi. Hivyo basi, lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu wenye kuongoza.”

Huu ni msingi wa tatu; usikivu na utiifu:

“… kusikiliza na kutii hata kama mtatawaliwa na mtumwa.”

Ni jambo lisilowezekana waislamu kuwa na umoja isipokuwa kwa kuwepo mtawala muislamu. Haijalishi kitu hata kama atakuwa kabila lake sio mwarabu. Bali hata kama atakuwa ni mwenye kumilikiwa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 18/05/2021