10. Msingi wa tatu: Kulingania kwa Allaah kwa ujuzi

3- Kulingania katika dini ya Allaah kwa elimu

Pindi Allaah atapomneemesha mtu elimu na matendo, basi aharakishe kuifikisha kheri hii kwa watu wengine kwa njia ya kuwalingania, kuwanasihi na kuwaelekeza. Hii ndio kazi ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Allaah (Ta´ala) amesema juu ya Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam):

قُلْ هَـٰذِهِ سَبِيلِي أَدْعُو إِلَى اللَّـهِ ۚ عَلَىٰ بَصِيرَةٍ أَنَا وَمَنِ اتَّبَعَنِي

”Sema: “Hii ndio njia yangu: nalingania kwa Allaah kwa ujuzi – mimi na anayenifuata.”[1]

Allaah ameinyanyua nafasi ya anayelingania Kwake juu ya wengine. Amesema (´Azza wa Jall):

وَمَنْ أَحْسَنُ قَوْلًا مِّمَّن دَعَا إِلَى اللَّـهِ وَعَمِلَ صَالِحًا وَقَالَ إِنَّنِي مِنَ الْمُسْلِمِينَ

“Na nani mwenye maneno mazuri zaidi kuliko yule anayelingania kwa Allaah na akatenda mema na akasema: “Hakika mimi ni miongoni mwa waislamu.”[2]

Kuhusu thawabu na ujira wake ni mkubwa kutokana na ukubwa wa kazi yake. Hakika yule anayelingania kwa Allaah anapata ujira sawa na yule anayemfuata katika jambo hilo la kheri pasi na kupungua chochote katika ujira wao[3]. Isitoshe imekuja katika Hadiyth ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) amesema:

“Kule Allaah kukuongozea mtu mmoja ni bora kwako kuliko ngamia wekundu[4].”[5]

[1] 12:108

[2] 43:33

[3] Muslim (2674).

[4] Ngamia wekundu kipindi hicho ndio ilikuwa mali tukufu zaidi kwa waarabu.

[5] al-Bukhaariy (4210) na Muslim (2406).

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Usuwl-ud-Da´wah as-Salafiyyah, uk. 36-37
  • Imechapishwa: 05/08/2020