Kuamini Qadar ina maana ya kuamini kuwa Allaah anayajua mambo yote – yaliyoko na yatayokuweko – na akayakadiria katika Ubao uliohifadhiwa na kwamba kila kinachopitika ni mamoja cha kheri na cha shari, kufuru, imani, utiifu na maasi, basi Allaah ametaka kiwe, amekikadiria na amekiumba. Hata hivyo anapenda utiifu na anachukia maasi. Pamoja na haya yote waja wana uwezo juu ya matendo yao, wana khiyari na utashi aidha katika ule utiifu au maasi yanayowapitikia. Lakini hayo yanakuja baada ya utashi na matakwa ya Allaah. Hili ni tofauti na Jabriyyah ambao wanasema kuwa mja ametenzwa nguvu juu ya matendo yake na kwamba hana khiyari yoyote. Vilevile ni tofauti na Qadariyyah ambao wanasema kuwa mja ana utashi unaojitegemea na kwamba anaumba matendo yake mwenyewe pasi na utashi wala matakwa ya Allaah. Allaah ameyaraddi hayo mapote yote mawili pale aliposema:

وَمَا تَشَاؤُونَ إِلَّا أَن يَشَاء اللَّهُ

“Wala nyinyi hamtataka isipokuwa atake Allaah.”[1]

Amewaraddi Jabriyyah waliopindukia pale alipomthibitishia mja kuwa na utashi. Amewaraddi Qadariyyah wakanushaji pale alipofanya kuwa utashi huo ni wenye kuja baada ya utashi wa Allaah.

Kuamini Qadar kunamfanya mja kuwa na subira juu ya majanga na kujiepusha na madhambi na misiba. Aidha kunampelekea mtu kutenda matendo na kujiepusha na kukata tamaa, kuwa na woga na kuzembea.

[1] 81:29

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min Usuwl ´Aqiydah Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 22-24
  • Imechapishwa: 12/05/2022