10. Msimamo sahihi juu ya Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat

Aayah nyingi za Qur-aan hazikosi kutaja majina na sifa za Allaah. Ukiongezea juu ya hilo kila Suurah imekuja kabla yake:

الرَّحِيمِ الرَّحْمَـٰنِ اللَّـهِ بِسْمِ

“Kwa jina la Allaah, Mwingi wa huruma, Mwenye kurehemu.”

Maana yake ni kumthibishia jina Allaah na kuthibitisha ya kwamba Yeye ni Mwingi wa huruma na ni Mwenye kurehemu. Vilevile kuna sifa nyingi mno za Allaah (´Azza wa Jall).

Allaah (Jalla wa ´Alaa) amejisifu Mwenyewe kwa sifa na vivyo hivyo Akajiita kwa majina. Kwa hivyo ni wajibu pia kwetu kumthibitishia hayo na wakati huohuo kuamini makusudio yaliyokusudiwa katika Qur-aan. Tusiingize akili zetu. Tusizipindishe maana kwa uelewa wetu. Tusimhukumu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Kwani Allaah ni mwenye kujijua Mwenyewe zaidi kuliko wanavyomjua wengine. Allaah (Jalla wa ´Alaa) anasema:

يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا

“Anajua yale yaliyoko mbele yao na yale yaliyoko nyuma yao na wala hawawezi kuzunguka kiujuzi.”[1]

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ الْحَيُّ الْقَيُّومُ ۚ لَا تَأْخُذُهُ سِنَةٌ وَلَا نَوْمٌ ۚ لَّهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ ۗ مَن ذَا الَّذِي يَشْفَعُ عِندَهُ إِلَّا بِإِذْنِهِ ۚ يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ ۖ وَلَا يُحِيطُونَ بِشَيْءٍ مِّنْ عِلْمِهِ إِلَّا بِمَا شَاءَ

“Allaah, hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, Aliyehai, msimamia kila kitu. Haumchukuwi usingizi wala kulala. Ni Vyake pekee vilivyomo katika mbingu na vilivyomo katika ardhi. Nani huyu ambaye anashufai mbele Yake bila ya idhini Yake. Anajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawawezi kuzunguka chochote katika elimu Yake isipokuwa kwa Alitakalo.”[2]

Allaah ametukataza kumpigia mifano, kumfanyia wenza, mawaziri na washirika. Kwa kuwa hakuna anayeshabihiana wala kufanana na Allaah. Hana washirika wala wenza – ametakasika na kuwa mbali kutokana na yale wanayomshirikisha.

Allaah (Jall wa ´Alaa) ametutaka sisi tumuabudu kwa kumuomba kwa majina na sifa Zake. Amesema (Ta´ala):

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Allaah ana majina mazuri kabisa, hivyo basi muombeni kwayo. Na waacheni wale wanaopotoa katika majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[3]

Hapa Allaah (Subhaanah) ametubainishia yafuatayo:

1 – Amejithibitishia Mwenyewe kuwa na majina:

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ

“Allaah ana majina mazuri kabisa.”

2 – Ameyasifu kuwa ni mazuri mno. Majina yote ya Allaah ni mazuri.

3 – Ametuamrisha kumuomba kwayo.

4 – Ametukataza kuyaharibu majina Yake.

Maana ya kuharibu (الإلحاد) ni kupinda. Kufanya uharibifu katika majina ya Allaah ni kupinda juu ya yale yanayofahamishwa kwayo ima kwa kuyapotosha au kuyapindisha maana kinyume na vile yanavyosema na ambavyo Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) hakukusudia. Hivi ndivyo wanavyofanya Jahmiyyah, Mu´tazilah na vifaranga vyao.

[1] 20:110

[2] 02:255

[3] 07:180

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mujmal ´Aqiydat-is-Salaf as-Swaalih, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 24/05/2022