33- Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufikwa na ufukara na akaupeleka kwa watu basi ufukara hautomtoka katu. Na akimpelekea nao Allaah, basi Allaah ima atampa utajiri kwa kipindi kifupi au atakufa haraka.”[1]

34- ´Abdur-Rahmaan bin Ma´n amesema:

“Hakuna mja yeyote mwenye kufikwa na tatizo na akamkimbilia Allaah isipokuwa Allaah humfariji.”

35 Ibraahiym bin Adham amesema:

“Kuwaomba watu haja ni pazia ilio kati yako wewe na Allaah (Ta´ala). Mpelekee haja zako Yule mwenye kudhuru na kunufaisha. Yafanye makimbilio yako yawe kwa Allaah na Allaah atakutosheleza na wengine wote na utaishi kwa furaha.”

36- al-Fudhwayl bin ´Iyaadhw amesema:

“Watu wenye kupendwa zaidi na watu ni wale wasiokuwa na haja na watu wengine na hawawaombi watu kitu. Watu wenye kuchukiwa zaidi na watu ni wale wenye kuwahitajia wengine. Watu wenye kupendwa zaidi na Allaah ni wale wenye kumuhitajia Allaah na kumuomba Yeye. Watu wenye kuchukiwa zaidi na Allaah ni wale wenye kujihisi kutomuhitajia Allaah na kutomuomba.”

[1] Abu Daawuud (1645), at-Tirmidhiy (2428), Ahmad (1/407) na wengine. Swahiyh kwa mujibu wa al-Haakim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 32-33
  • Imechapishwa: 18/03/2017