10. Mjadala wa Mtume na wakristo wa Najraan

Ndipo akanambia: “Katika Qur-aan kuna mgongano pia. Katika sura al-Maa´idah” imekuja:

وَلْيَحْكُمْ أَهْلُ الْإِنجِيلِ بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فِيهِ

“Kwa hiyo wale wenye kufuata Injili wahukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah ndani yake.” (05:47)

Hata hivyo katika “Aal ´Imraan” imekuja:

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake naye Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (03:85)

Vipi tutaweza kuoanisha kati ya Aya hizi mbili?” Nikafikiria kidogo na nikajibu kutokamana na msukumo kutoka kwa Allaah: “Kabla ya kujibu juu ya pingamizi hii ni wajibu kwetu kujua mzozo kati ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakristo na ilikuwa inahusiana na nini. Akasema: “Sema wewe.” Nikasema: “Inahusiana na ´Iysaa bin Maryam. Wakristo wa Najraan walikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumtuhumu ya kwamba anawatukania mtu wao. Alipowauliza ni yupi wanayemaanisha wakasema: “´Iysaa bin Maryam.” Alipowauliza anamtukana vipi wakasema kumwambia: “Unasema kuwa ni mtu wa kawaida na sio mwana wa Allaah.” Akawa amejadiliana nao na akawabainishia hoja, lakini hata hivyo wakaendelea kukaidi. Ndipo Allaah akateremsha:

إِنَّ مَثَلَ عِيسَىٰ عِندَ اللَّـهِ كَمَثَلِ آدَمَ ۖ خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُن فَيَكُونُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ فَلَا تَكُن مِّنَ الْمُمْتَرِينَ

“Hakika mfano wa ‘Iysaa kwa Allaah ni kama mfano wa Aadam. Amemuumba kutokana na udongo kisha akamwambia: “Kuwa!” na akawa. Haki kutoka kwa Mola wako, basi usiwe miongoni mwa wanaotia shaka. (03:59-60)

Walipoendelea kung´ang´ania ya kwamba ni mwana wa Allaah na ni mmoja katika utatu, Allaah akamwamrisha awape changamoto wamuombe Allaah amlaani yule mwenye kusema uongo. Wakaogopa kufanya hivo na wakafanya mkataba wa amani. Ilikuwa ni kuhusiana na mjadala huu Allaah (Ta´ala) akateremsha:

وَلْيَحْكُمْ أَهْلُ الْإِنجِيلِ بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فِيهِ

“Kwa hiyo wale wenye kufuata Injili wahukumu kwa yale aliyoyateremsha Allaah ndani yake.” (05:47)

Kuja kwa wakristo wa Najraan kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuswali kwenye msikiti wake kwa idhini yake ni jambo limetajwa kwenye vitabu vya Hadiyth na vya historia.

  • Mhusika: ´Allaamah Muhammad Taqiyy-ud-Diyn al-Hilaaliy al-Maghribiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Baraahiyn al-Injiylyyah ´alaa anna ´Iysaa daakhil fiyl-´Ubuudiyyah wa la hadhdhwa lahu fiyl-Uluuhiyyah, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 16/10/2016