10. Misingi mitano ya Mu´tazilah na ukati kati wa Ahl-us-Sunnah


Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kundi lililookoka liko kati na kati katika mlango wa matendo ya Allaah baina ya Qadariyyah na Jabriyyah.”

MAELEZO

Wakati Shaykh (Rahimahu Allaah) mwanzoni mwa kitabu alipotaja misingi ya imani ambayo ni kumwamini Allaah, Malaika Wake, Vitabu Vyake, Mitume Yake, siku ya Mwisho na kuamini Qadar kheri na shari yake na akabainisha kuwa yuko katika ´Aqiydah ya Salaf katika majina na sifa Zake akiwa ni mwenye kwenda kinyume na pote la Mu´attwilah, Mushabbihah na Mumaththilah na akathibitisha msingi huu ambao unaingia katika kumwamini Allaah (´Azza wa Jall). Kwa sababu kumwamini Allaah kunajumuisha kuamini Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah, kuamini Tahwiyd-ul-Uluuhiyyah na kuamini Tawhiyd-ul-Asmaa´ was-Swifaat. Kisha katika sentesi hii akataja yanayohusiana na msingi wa mwisho ambao ni kuamini Qadar. Kwa sababu kumetokea tofauti na kutengana kati ya pote la Qadariyyah na pote la Jabriyyah.

Qadariyyah ni wale waaopinga Qadar. Nao ni Mu´tazilah wafuasi wa Waaswil bin ´Atwaa´. Wameitwa hivo kwa sababu walijitenga na kikao cha al-Hasan al-Baswriy (Rahimahu Allaah) na wakawa na wafuasi na wakajenga madhehebu katika Tawhiyd yanayokwenda kinyume na madhehebu ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Vilevile katika misingi ya imani wamejiwekea misingi mingine. Nayo ni misingi mitano:

Wa kwanza: Tawhiyd: Makusudio yao ni kupinga sifa za Allaah. Kitendo chao cha kupinga sifa wanaita kuwa ni “Tawhiyd”. Kwa sababu wanaona kuthibitisha sifa za Allaah kunapelekea kuwepo kwa waugu wengi.

Wa pili: Uadilifu: Wanachokusudia ni kupinga mipango na makadirio. Kwa sababu wanaamini kuwa kuthibitisha mipango na makadirio kunapelekea ukandamizaji na dhuluma kwa Allaah (Ta´ala). Kwa sababu atakuwa amewaadhibu waja Wake kwa kitu ambacho tayari amekwishawakadiria.

Wa tatu: Kuamrisha mema na kukataza maovu: Wanachokusudia ni kujivua katika utiifu wa watawala. Wanaona kuwa yule anayewafanyia uasi watawala ndiye ambaye anaamrisha mema na kukataza maovu.

Wa nne: Nafasi ilio kati ya nafasi mbili: Sababu hii ndio ilimfanya kwenda kinyume na kujitenga na kikao cha al-Hasan al-Baswriy. Wakati al-Hasan al-Baswriy (Rahimahu Allaah) alipoulizwa hukumu ya muislamu mwenye kutenda dhambi kubwa akajibu kwa mujibu wa ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah ambapo akasema:

“Ni muumini mwenye imani pungufu.”

Hawamkufurishi kama ambavo Khawaarij wanamkufurisha kama ambavo hawamsifii imani kamilifu kama wanavooona Murji-ah. Bali ni muumini mwenye imani pungufu. Ni muumini kwa imani yake na ni mtenda dhambi kwa dhambi yake kubwa. Pindi al-Hasan al-Baswriy alipojibu kwa jawabu hili na Waaswil bin ´Atwaa´ alikuwa ni mwanafunzi wake akasema:

“Mimi nasema kwamba sio muumini na wala sio kafiri. Bali yuko katika sehemu baina ya sehemu mbili.”

Anatoka nje ya imani lakini wakati huohui haingii ndani ya ukafiri. Yuko katika sehemu baina ya sehemu mbili. Sio muumini na wala sio kafiri. Akifa bila ya kutubia atadumishwa Motoni milele, kama wanavoamini Khawaarij. Hivyo wakazusha kauli ya sehemu kati ya sehemu mbili na wakakubali hilo[1].

Wa tano: Kutimiza ahadi: Wanachokusudia ni kwamba Motoni hatotoka ndani yake yule mwenye kuuingia. Hivyo wakalazimisha kumdumisha Motoni yule muislamu mwenye kutenda dhambi kubwa na wakasema kwamba yule mwenye kustahiki adhabu hastahiki thawabu.

[1] Tazama ”al-Milal wan-Nihal” (01/48) ya ash-Sharastaaniy na ”Siyar A´laam-in-Nubalaa´” (05/464).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh ´Aqiydat-il-Imaam Mujaddid Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab, uk. 28-29
  • Imechapishwa: 03/03/2021