10. Mfano wa pili wa hekima ya Mtume (صلى الله عليه وسلم)

Ni kuhusu yule swahabah aliyemwingilia mke wake mchana wa Ramadhaan. al-Bukhaariy na Muslim wamepokea kupitia Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia ya kwamba kuna mtu alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Nimeangamia.” Akamuuliza: “Ni kipi kimechokuangamiza?” Akajibu: “Nimemwingilia mke wangu [mchana wa] Ramadhaan ilihali nimefunga.”

Hii ni dhambi kubwa mtu akakusudia kumwingilia mke wake mchana wa Ramadhaan ilihali amefunga. Ni kipi alichomfanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam); alimshtua, alimtukana au alimkemea? Hapana. Kwa kuwa mwanaume huyu amekuja hali ya kuwa ni mwenye kutubia na kujuta. Si ambaye anapuuzia yale yaliyomtokea. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamuuliza:

“Je, una mtumwa uwezaye kumwacha huru ikiwa ni kafara ya uliyofanya?” Akasema: “Hapana.” Akamuuliza: “Je, unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?” Akasema: “Hapana.” Akamuuliza: “Je, unaweza kulisha masikini sitini?” Akasema: “Hapana.” Mtu yule akaketi chini. Tahamaki Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaja na tende na kumwambia: “Chukua hizi na uzitoe swadaqah.” Akamwambia: “Hivi kweli kuna fakiri uliko mimi, ee Mtume wa Allaah?” Ninaapa kwa Allaah! Hakuna kati ya nyumba hizi ambaye ni fakiri kuliko mimi.” Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akacheka mpaka yakaonekana magego yake. Halafu akasema: “Basi walishe familia yako.”

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dawr-ul-Mar´ah fiy Iswlaah-il-Mujtama´ https://www.sahab.net/home/?p=806
  • Imechapishwa: 02/02/2017