Tuwatazame watu hawa ambao wanamwabudu Allaah kwa Bid´ah namna walivyokuwa makundi-makundi yakikufurishana na yakitiana kwenye ufuska na wakati huohuo wote wanajiita kuwa ni ´waislamu`. Wako ambao wamewakufurisha baadhi ya watu kwa mambo yasiyompelekea mtu kwenye ukafiri. Lakini si vyengine isipokuwa ni matamanio ndio yamewafanya vipofu na kuyaziba macho yao.

Tukifuata mwenendo huu ambapo hatumwabudu Allaah isipokuwa kwa yale yaliyomo ndani ya dini ya Allaah basi hakika tutakuwa Ummah mmoja tu. Iwapo tutamwabudu Allaah (Ta´ala) kwa Shari´ah na mwongozo Wake basi tutakuwa Ummah mmoja. Shari´ah ya Allaah ni mwongozo na sio matamanio.

Akipatikana mmoja katika Ahl-ul-Bid´ah ambaye anazusha mrengo wa kiimani au wa kimaneno – ni mamoja yakawa maneno au vitendo – na akasema kuwa ni jambo zuri kwa kutumia dalili ya maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Atakayehuisha katika Uislamu mwenendo mzuri basi atapata ujira wake na ujira wa atakayeutendea kazi hadi siku ya Qiyaamah.”[1]

Tutamuuliza kwa kifua kipana: je, jambo zuri hili ulilodai kwamba limethibiti katika Bid´ah hii lilikuwa limefichikana kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au alikuwa analijua lakini hata hivyo akalificha na hakuna yeyote katika Salaf ambaye alilijua mpaka ukaja wewe kulijua?

Akijibu jibu la kwanza ni shari na akijibu jibu ni la pili shari zaidi. Akisema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakujua uzuri wa jambo hili na ndio maana halikuweka katika Shari´ah, basi tutamwambia kwamba amemtuhumu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) jambo kubwa. Hiyo ina maana kwamba amemfanya kuwa ni mjinga juu ya dini na Shari´ah ya Allaah. Akisema kuwa alilijua lakini akawaficha nalo waja, basi hili ni la kutisha na chungu zaidi. Hiyo ina maana kwamba amemsifu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) – ambaye ni mwaminifu na mkarimu – kufanya ukhaini na kutotaka kuitoa elimu yake. Hili ni la shari zaidi kwa vile si mwenye kutaka kuitoa ellimu yake. Pamoja na kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa ni mkarimu zaidi wa watu. Kuna uwezekano wa tatu ambao ni shari vilevile ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilijua na akalifikisha jambo hilo lakini hata hivyo halikutufikia. Tunamjibu kwa kusema kwamba amebeza maneno ya Allaah (´Azza wa Jall) kwa vile amesema (Ta´ala):

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

“Hakika Sisi Tumeteremsha hii Qur-aan na hakika Sisi bila shaka ndio Tutakaoihifadhi!”[2]

Shari´ah moja wapo ya Ukumbusho ikipotea maana yake ni kwamba Allaah hakuihifadhi. Bali kuna upungufu katika kuihifadhi Kwake kwa kiwango cha kitachokuwa kimekosekana kutoka katika Shari´ah hiyo ambayo Ukumbusho huu umeteremka kwa ajili yake.

[1] Muslim.

[2] 15:09

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Manhaj Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah fiy-´Aqiydah wal-´Amal, uk. 19-23
  • Imechapishwa: 14/07/2019