Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Dalili ya waja wema ni maneno Yake (Ta´ala):

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ وَيَرْجُونَ رَحْمَتَهُ وَيَخَافُونَ عَذَابَهُ

“Hao wanaowaomba [wao wenyewe] wanatafuta kwa Mola wao njia [na] kumkurubia kadri wanavyoweza na wanataraji rehema Zake na wanakhofu adhabu Yake.” (17:57)

MAELEZO

Hapa kunatajwa dalili yenye kuonesha kuwa kuna wenye kuabudu watu wema:

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ

“Hao wanaowaomba [wao wenyewe] wanatafuta kwa Mola wao njia [na] kumkurubia kadri wanavyoweza… “

Kuna maoni yanayosema kuwa Aayah hii imeteremshwa kwa wale wenye kumwabudu al-Masiyh, mama yake na ´Uzayr. Ndipo (Subhaanah) akakhabarisha kuwa al-Masiyh, mama yake Maryam na ´Uzayr kuwa wote ni waja wa Allaah. Wanajaribu kujikurubisha kwa Allaah, wanatarajia huruma Yake na wanaogopa adhabu Yake. Wao wenyewe ni waja wanaomuhitajia Allaah, wanamwomba na wanafanya Tawassul Kwake kwa kumtii:

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يَدْعُونَ يَبْتَغُونَ إِلَىٰ رَبِّهِمُ الْوَسِيلَةَ أَيُّهُمْ أَقْرَبُ

“Hao wanaowaomba [wao wenyewe] wanatafuta kwa Mola wao njia [na] kumkurubia kadri wanavyoweza… “

Bi maana kujikurubisha Kwake (Subhaanah) kwa kumtii na kumuabudu. Hii ina maana ya kwamba wao wenyewe ni wahitaji na mafukara wenye kumuomba Allaah, wanatarajia huruma Yake na wanaogopa adhabu Yake. Kwa ajili hiyo hawastahiki kuabudiwa kwa kuwa ni wanaadamu.

Maoni mengine yanasema kuwa [Aayah hii] imeteremshwa juu ya kundi la washirikina waliokuwa wakiyaabudu majini. Baada ya hapo majini haya yakasilimu na wale wenye kuwaabudu hawakutambua juu ya kusilimu kwao. Yakawa yanajikurubisha kwa Allaah, yanatarajia huruma Yake na kuchelea adhabu Yake. Kwa hivyo wao wenyewe ni wahitaji na mafukara wasiostahiki kuabudiwa.

Pasi na kujali malengo ya Aayah hii tukufu, inafahamisha kuwa haijuzu kuwaabudu waja wema. Ni mamoja wakawa ni Mitume, wakweli, mawalii au waja wema. Haijuzu kuwaabudu, kwa sababu wote ni waja mafukara wa Allaah, wenye kumuhitajia. Ni vipi basi wataabudiwa pamoja na Allaah (Jalla wa ´Alaa)?

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qawaa´id al-Arba´ah, uk. 26-27
  • Imechapishwa: 18/08/2022