10. Kujitokeza kwa ad-Dajjaal


al-Masiyh ad-Dajjaal ni al-Masiyh wa upotofu ambaye atajitokeza katika zama za mwisho. Kujitokeza kwake ni katika alama za Qiyaamah. Ameitwa hivo kwa sababu ya jicho moja. Kuna maoni mengine yanayosema kuwa ameitwa hivo kwa sababu ya kutembea kwake kwa kasi ulimwenguni. Ni mwenye chongo na al-Masiyh wa upotofu. Hakuna Mtume yeyote isipokuwa aliwatahadharisha Ummah wake juu yake. Hata hivyo matahadharisho ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yalikuwa makubwa zaidi kuliko Mitume wengine kwa sababu atakuwepo karibu zaidi na zama zake kuliko waliomtangulia.

Atajitokeza mwishoni mwa zama za Qiyaamah na atafuatwa na mayahudi. Kisha atateremka al-Masiyh wa uongofu ´Iysaa bin Maryam (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na atamuua ad-Dajjaal huyu Ludd huko Palestina. Hapo ndipo Allaah atawasalimisha waislamu kutokamana na shari zao, waislamu wawashinde mayahudi, hukumu ya Uislamu ishinde juu ya ardhi na haki ienee. Lakini hayo yatakuwa baada ya mitihani na matatizo.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametuwekea katika Shari´ah kuomba ulinzi kutokamana naye katika kila Tashahhud mwishoni mwa kila swalah kwa kusema:

اللَّهُمَّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ مِنْ عَذَابِ جهنم و من عَذَابِ الْقَبْر ومِنْ فِتْنَةِ الْمَحْيَا وَالْمَمَاتِ وَ مِنْ شرِ فتنة الْمَسِيحِ الدَّجَّالِ

“Ee Allaah! Hakika mimi najilinda Kwako kutokamana na adhabu ya Jahannam, kutokaman na adhabu ya kaburi, kutokamana na mtihani wa uhai na kifo na kutokamana na shari ya al-Masiyh ad-Dajjaal.“[1]

[1] Muslim (1324) na Ahmad (10180).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 446
  • Imechapishwa: 03/09/2019