7- Baadhi yao wafanye haraka kulipa madeni yake kutoka katika mali yake hata kama itapelekea kuitoa yote. Asipokuwa na mali basi ni lazima kwa dola kumtolea akiwa alifanya bidii katika kuyalipa. Dola isipofanya hivo na baadhi ya watu wakajitolea inafaa. Kuhusu hilo kumekuja baadhi ya Hadiyth:

Ya kwanza: Sa´d bin al-Atw-wal (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Kwamba ndugu yake alikufa na ameacha dirhamu  mia tatu na ameacha familia ambapo nikataka kuzitoa kuwapa familia yake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akanambia:

“Hakika kaka yako amewekwa kizuizini kwa sababu ya deni lake. [Nenda] umlipie nalo. [Nikaenda na kumlipia nalo kisha nikaja] na kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Nimemlipia nalo isipokuwa tu dinari mbili zilizodaiwa na mwanamke mmoja na wala hana ushahidi. Akasema: “Hakika ni mkweli.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Amesema ukweli.”

Ameipokea Ibn Maajah (02/82), Ahmad (04/136, 05/07), al-Bayhaqiy (10/142), Ahmad kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Nyingine ni kama mfano wa cheni ya wapokezi ya Ibn Maajah. Ameisahihisha al-Buuswayriy katika “az-Zawaaid”. Mtiririko wa Hadiyth na upokezi wa pili ni wa al-Bayhaqiy. Nayo na ziada ni za Ahmad katika upokezi mmoja.

Ya pili: Samurah bin Jundub ameeleza.

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliiswalia jeneza.”

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Aliswali Subh.”

Wakati alipomaliza akasema: “Je, kuna yeyote wa watu wa familia ya fulani yuko hapa?” [Wakanyamaza. Walikuwa wanapoanzwa kwa jambo hunyamaza]. Akauliza hivo mara nyingi [mara tatu pasi na kujibiwa na yeyote]. [Bwana mmoja akasema: “Huyu hapa]. Akasimama mtu mmoja akiwa anaburuza kikoi chake kutoka mwishonimwishoni mwa watu [Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ni kipi kilichokuzuia kujibu zile mara mbili za mwanzo?] Hakika mimi sikutaja kutaja jina lako waziwazi isipokuwa kwa kheri. Hakika fulani – ambaye ni katika watu miongoni mwao – amezuiliwa kwa sababu ya deni lake [kutokamana na Pepo. Kama mnaweza mkomboeni na mkitaka msalimisheni kwenye adhabu ya Allaah]. Yalaiti ungeliwaona familia yake na wale wenye kuchunga jambo lake walivosimama na wakamlipia nalo [mpaka hakukuweko mwengine anayemdai chochote][1].

Ameipokea Abu Daawuud (02/84), an-Nasaa´iy (02/233), al-Haakim (02/25,26), al-Bayhaqiy (06/04/76), at-Twayaalisiy katika “al-Musnad” yake (nambari. 891, 892), vilevile Ahmad (05/11, 13, 20). Baadhi yao wamepokea kupitia kwa Sha´biy kutoka kwa Samurah na wengine wameingiza kati yake Sam´aan bin Mushannaj. Kwa njia ya kwanza ni Swahiyh juu ya sharti za al-Bukhaariy na Muslim, kama alivosema al-Haakim na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Kwa njia ya pili ni Swahiyh tu.

Upokezi mwingine ni kwa zile “Musnad” mbili, ziada ya kwanza na ziada ya pili ni ya al-Haakim, vilevile ziada ya tatu na ya tano, al-Bayhaqiy ni hiyo ya pili, Ahmad ni hiyo ya tatu na ya nne, at-Twayaalisiy ni hiyo ya tano. Anayo yeye, Ahmad na Abu Daawuud hiyo ziada ya sita.

Ya tatu: Jaabir bin ´Abdillaah amesimulia kwa kusema:

“Kuna mtu mmoja amekufa ambapo tukamuosha, tukamvika, tukampaka mafuta ya maiti na tukamuweka kwa ajili ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) sehemu inapowekwa jeneza kunapoitwa “Maqaam Jibriyl”. Kisha tukamjulisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili amswalie. Akaja pamoja nasi [akapiga hatua] kadhaa kisha akasema: “Huenda mwenzenu huyu anadaiwa?” Wakasema: “Ndio, dinari mbili.” Akarudi nyuma. [Akasema: “Mswalieni mwenzenu]. Mtu mmoja katika sisi akiitwa Abu Qataadah akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Nachukua jukumu hilo. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa anasema: “Liko kwa jukumu lako na zitatoka katika mali yako na maiti yuko nazo mbali?” Akasema: “Ndio.” Akamswalia na ikawa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akikutana na Abu Qataadah akisema: [Katika upokezi mwingine imekuja kwamba alikutana naye siku ya kufuata akasema:] “Umefanya nini kwa dinari zile mbili?” [Akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Amekufa tu jana] mpaka ukafika mwisho wa hilo [Katika upokezi mwingine: “Kisha akakutana naye siku inayofuata akasema: “Zimefanyaje dinari zile mbili?”] Akasema: “Nimezilipa, ee Mtume wa Allaah. Akasema: “Hivi sasa ndio imepozwa ngozi yake.”[2]

Ameipokea al-Haakim (02/58) na mtiririko ni wake, na al-Bayhaqiy (06/74-75), at-Twayaalisiy (1673), Ahmad (03/330) kwa cheni ya wapokezi nzuri, kama alivosema al-Haythamiy (03/39). Kuhusu al-Haakim amesema:

“Ni yenye cheni ya wapokezi Swahiyh” na adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

Mapokezi mengine na ziada ni za kwao wote isipokuwa al-Haakim. Isipokuwa ziada ya pili ni ya at-Twayaalisiy mwenyewe.

[1] Ina ushahidi kutoka katika Hadiyth ya Ibn ´Abbaas. Ameipokea at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (q. 02/156) kwa cheni ya wapokezi dhaifu.

[2] Bi maana imekuwa ni sababu ya kuondolewa adhabu baada ya kulilipa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ahkaam-ul-Janaa-iz wa Bid´ahaa, uk. 25-27
  • Imechapishwa: 26/12/2019