10. Kufunga safari kwenda katika makaburi ya waja wema

Swali: Watu wengi wanafunga safari kwenda katika makaburi ya waja wema hali ya kuwaomba wenye nayo kuwaponya wagonjwa wao au kutatua mahitaji yao na wanawatekelezea wenye makaburi hayo nadhiri na vichinjwa. Aidha wanawaomba, wanawataka uokozi na matendo mfano wa mambo hayo. Maoni yametofautiana juu ya suala hili; wanaofanya matendo hayo wanasema kuwa Allaah ulimwenguni yuko na waja ambao anaitikia du´aa kwa ajili yao. Wanaopingana na kitendo hichi wanasema kuwa ni shirki ya wazi na inamtoa mwenye nayo nje ya dini. Tunataraji utatupa mwanga zaidi juu ya vipengele vya maudhui pamoja na kutubainishia kama inafaa kuswali nyuma ya anayefanya hivo au haifai?

Jibu: Swali hili ni muhimu na kubwa mno. Linahusu kufunga safari kuyaendea makaburi kwa ajili ya kuwaomba wenye nayo mahitajio mbalimbali, wawaponyeshe wagonjwa, kuwaomba wakuombee, kuwawekea nadhiri, kuwachinjia na mfano wa hayo.

Kuhusu kile kitendo cha kufunga safari kwa ajili ya kuyatembelea makaburi haifai kwa mujibu wa maoni sahihi zaidi ya wanazuoni. Kwa sababu imekatazwa na nia njia inayopelekea katika shirki. Msingi wa hili ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Kusifungwe safari isipokuwa kuelekea katika misikiti mitatu; msikiti Mtakatifu, msikiti huu – yaani msikiti wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) uliopo Madiyna – na msikiti wa al-Aqswaa.”[1]

Misikiti hii mitatu inafungiwa safari kwa andiko la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Mbali na hii haifungiwi safari. Kwa hivyo kunaingia katika hilo misikiti mingine iliobaki na makaburi yana haki zaidi ya kutofaa. Ikiwa haifai kufunga safari kwenda katika misikiti – ambayo ndio maeneo bora zaidi – basi maeneo mengine ambayo yanafungiwa safari kwa ajili ya ubora wa yule aliyezikwa basi kuna haki zaidi ya kuzuiwa. Kwa ajili hiyo maoni sahihi zaidi ya wanazuoni ni kwamba ni haramu kufunga safari kuyatembelea makaburi. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yatembeleeni makaburi. Kwani hakika yanakukumbusheni Aakhirah.”[2]

Sunnah ni kuyatembelea makaburi na kuwaombea wenye nayo msamaha na rehema kwa wanamme peke yao pasi na wanawake. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kuyatembelea makaburi na akasema kuwa kunakumbusha mtu na kifo na Aakhirah. Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiwafunza Maswahabah zake jambo hilo na akiwafunza pindi wanapoyatembelea makaburi waseme:

السلام عليكم أهل الديار من المؤمنين والمسلمين وإنا إن شاء الله بكم لاحقون نسأل الله لنا ولكم العافية

“Amani ya Allaah iwe juu yenu wakazi waumini na waislamu. Nasi – Allaah akitaka – tutaungana na nyinyi. Tunamuomba Allaah juu yetu sisi na nyinyi afya.”[3]

Yeye mwenyewe (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akitembelea al-Baqiy´, akiwaombea rehema na msamaha. Kuhusu kuyafungia safari haifai. Haifai kufunga safari kwa ajili ya kuyatembelea makaburi kama ambavo haifai kufunga safari kwa ajili ya kuitembelea misikiti mingine mbali na ile misikiti mitatu.

Lakini ikiwa kwa kufunga kwake safari atakusudia kumwomba na kumtaka uokozi yule maiti, basi itambulike kuwa hayo ni maovu na haramu kwa maafikiano ya waislamu. Haijalishi kitu hata kama atayafanya hayo pasi na kufunga safari. Akiyaendea makaburi yaliyopo mjini mwake pasi na kufunga safari ambapo akawaomba uokozi, akawawekea nadhiri, akawachinjia, akawaomba kutatuliwa haja kama vile kuwaponya wagonjwa au kuwaondoshea majanga, hiyo itakuwa ni shirki kubwa na shirki ya wazi. Hii ndio shirki ya wale wa mwanzo kabla ya kuja Uislamu. Walikuwa wakiyafanya hayo kwa wafu wao. Kipindi cha kishirikina walikuwa wakiwashirikisha wafu ambapo wakiwaomba uokozi na wakiwawekea nadhiri na wakisema:

هَـٰؤُلَاءِ شُفَعَاؤُنَا عِندَ اللَّـهِ

“Hawa ni waombezi wetu mbele ya Allaah.”[4]

مَا نَعْبُدُهُمْ إِلَّا لِيُقَرِّبُونَا إِلَى اللَّـهِ زُلْفَىٰ

“Hatuwaabudu isipokuwa ili wapate kutukurubisha kwa Allaah karibu.”[5]

 Shirki maana yake ni kutekeleza baadhi ya ´ibaadah kumfanyia asiyekuwa Allaah. Mfano wa ´ibaadah hizo ni kama du´aa, khofu, kutaraji, kutegemea, kuchinja, nadhiri, swalah au swawm. Ambaye anawaomba wafu, anawataka uokozi na anawawekea nadhiri na huku anadai kuwa watamwombea au watamkurubisha mbele ya Allaah amefanya kitendo cha washirikina wa mwanzo sambamba. Vivyo hivyo akijikurubisha mbele yao kwa kuwachinjia na kuwawekea nadhiri,  yote hayo ni kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall). Yote ni maovu. Ni lazima kwa wanazuoni kuyakataza, kubainisha upotofu wake na kutahadharisha wajinga kutokamana na matendo hayo. Shirki kama hiyohiyo ndio imefanywa na Abu Jahl na watu mfano wake katika kipindi cha kishirikina kwa al-Laat, al-´Uzza na Manaat. Hii ndio shirki ya wale wa mwanzo kwa masanamu na mizimu yao kila mahali.

Miongoni mwa majanga ni wajinga wafikiri kuwa matendo hayo ni dini au kujikurubisha na wayanyamazie mambo hayo wale wanaojinasibisha na elimu na wachukulie wepesi mambo hayo. Haya yanawadhuru wajinga kudhukuru kukubwa pale ambapo watanyamaza wale wanaojinasibisha na elimu na wasikemee shirki hii basi wajinga watadhani kuwa inafaa, kwamba ni dini na kwamba ni kujikurubisha. Matokeo yake watabaki na kuendelea na mambo hayo.

Kwa hivyo ni lazima kwa wanazuoni kukemea kumshirikisha Allaah, kukemea Bid´ah na kukemea maasi na kutahadharisha mambo hayo na kuwazindua wale watu wa kawaida juu ya yale yote ambayo Allaah amewaharamishia ili wajiepushe nayo kuanzia shirki na yaliyo chini yake.

Hapana shaka yoyote kwamba kuwaomba wafu, kuwataka uokozi, wakuponyee wagonjwa na wakusaidie ndio kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall). Mambo haya yanafanywa na watu wengi kwenye makaburi, kama wanavofanya baadhi ya watu kwenye kaburi la Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) masiku ya hajj na baadhi ya wajinga. Kama pia wanavofanya watu wengi kwenye kaburi la bwana al-Badawiy huko Misri, kaburi la al-Husayn huko Misri na makaburi mengine. Vivyo hivyo ndivo wanavofanya karibu na kaburi la Shaykh ´Abdul-Qaadir al-Jaylaaniy. Yanafanywa na baadhi ya watu ilihali wako mbali na makaburi haya. Wanawaomba kutokea kwa mbali na wanawaomba kuwatatulia haja na kuwaponya wagonjwa kutokea kwa mbali. Haya pia yanafanyika kwenye makaburi ya watu wa nyumbani kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka kwa baadhi ya wale wanaoyatembelea ambao ni Shiy´ah na wengineo. Vivyo hivyo karibu na kaburi la Ibn ´Arabiy huko Shaam. Hali kadhalika katika makaburi mengine katika nchi asizojua hesabu yake isipokuuwa Allaah (´Azza wa Jall). Hili ndio janga kubwa, shari yake imeenea na madhara yake yamekuwa makubwa kutokana na sababu ya uchache wa elimu na uchache wa wenye kuzindua juu ya jambo hili la khatari.

Mimi nawalingania wanazuoni wote kila mahali wamche Allaah, wawaonye watu juu ya shirki hii, wawatahadharishe na wawabainishie kuwa ´ibaadah ni haki ya Allaah pekee. Amesema (Subhaanah):

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.”[6]

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”[7]

وَاعْبُدُوا اللَّـهَ وَلَا تُشْرِكُوا بِهِ شَيْئًا

“Na mwabuduni Allaah na wala msimshirikishe Yeye na chochote.”[8]

فَاعْبُدِ اللَّـهَ مُخْلِصًا لَّهُ الدِّينَ أَلَا لِلَّـهِ الدِّينُ الْخَالِصُ

“Mwabudu Allaah hali ya kumtakasia Yeye dini. Zindukeni! Ni ya Allaah pekee dini iliyotakasika.”[9]

وَأَنَّ الْمَسَاجِدَ لِلَّـهِ فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hakika misikiti yote ni ya Allaah, hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[10]

Zipo Aayah nyingi zinazojulisha ulazima wa kumtakasia ´ibaadah Allaah peke yake na kwamba haijuzu kabisa kumwabudu yeyote badala Yake miongoni mwa miti, wafu, masanamu, nyota na venginevyo. ´Ibaadah ni haki ya Allaah pekee. Si haki ya mwengine yeyote; si Malaika, Mitume, waja wema wala wengineo. Bali ´ibaadah ni haki ya Allaah pekee. Mitume wametumwa ili wawafunze watu dini yao, wawatahadharishe kumshirikisha Allaah na kuwaelekeza kumwabudu Allaah pekee. Amesema (Subhaanah):

وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ

”Hakika Tulituma katika kila ummah Mtume kwamba: “Mwabuduni Allaah na jiepusheni na Twaaghuut [waungu batili].”[11]

وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ مِن رَّسُولٍ إِلَّا نُوحِي إِلَيْهِ أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدُونِ

“Hatukutuma kabla yako Mtume yeyote isipokuwa Tulimfunulia Wahy ya kwamba: “Hakika hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Mimi; hivyo basi niabuduni.”[12]

Zipo Aayah nyingi zengine.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia Mu´aadh:

“Je, unaijua haki ya Allaah juu ya waja na haki ya waja juu ya Allaah Nikasema: “Allaah na Mtume Wake ndio wanajua zaidi.” Akasema: “Haki ya Allaah juu ya waja ni wamwabudu Yeye na wasimshirikishe na chochote. Na haki ya waja juu ya Allaah ni asimwadhibu yule ambaye hakumshirikisha na chochote.”

Hizo ni haki mbili; haki ya Allaah juu ya waja na haki ya waja juu ya Allaah. Kuhusu haki ya Allaah juu ya viumbe ni haki ya lazima na kuu. Ni lazima waitekeleze kwa sababu wameumbwa kwa ajili yake. Amesema (Subhaanah):

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ

“Sikuumba majini na wana Aadam isipokuwa waniabudu.”[13]

Allaah amewatumiliza Mitume kwa ajili yake kama tulivotangulia kusema. Kwa hivyo ni lazima kwa viumbe wamwabudu Allaah pekee. Hii ni haki inayowalazimu na ni haki aliyowafaradhishia. Hivyo ni lazima waitekeleze na ni lazima watekeleze yale yote ambayo Allaah amewaamrisha na Mtume Wake na wajiepushe na yale yote ambayo Allaah amewagombeza na Mtume Wake. Kufanya yote haya ni katika kumwabudu (Subhaanahu wa Ta´ala); kutekeleza yale ya faradhi, kujiepusha na yale ya haramu, kutafuta uso wa Allaah na kumtakasia Yeye nia. Yote haya ni katika kumwabudu, kumtii na kumtukuza.

Kuhusu haki ya waja juu ya Allaah ni haki ya kuwafanyia wema na ukarimu. Miongoni mwa ukarimu, utoaji na wema Wake ni kwamba yule atakayekutana Naye hali ya kuwa anamwabudu Yeye pekee, anamwamini na ameongoka, basi Allaah atamwingiza Peponi na hatomwingiza Motoni. Hii ni fadhilah na wema Wake (Jalla wa ´Alaa). Amesema (Subhaanah):

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَهُمْ جَنَّاتُ النَّعِيمِ

“Hakika wale walioamini na wakafanya mema watapata mabustaani yenye neema.”[14]

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَنَعِيمٍ

“Hakika wale wenye kumcha Allaah watakuwa katika mabustani yenye neema.”[15]

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ

“Hakika wale wenye kumcha Allaah watakuwa katika mabustani na chemchemu.”[16]

Kwa hivyo ni lazima kwa waislamu kumwabudu Allaah pekee, wamkhusishe kwa ´ibaadah na wawe na ufahamu katika dini ya Allaah na watahadhari kumshirikisha Allaah. Madai ya Uislamu pamoja na kupatikana kwa shirki hayafai kitu. Bali Uislamu wake unachenguka kwa kule kumshirikisha Kwake Allaah. Bali shirki inachengua na kubatilisha Uislamu. Kwa hivyo ni lazima kwa wale wanaojinasibisha na Uislamu wauhakiki Uislamu wao, wawe na ufahamu katika dini ya Allaah na wahifadhi dini Yake kwa aina mbalimbali za kumshirikisha Allaah (´Azza wa Jall) ili uweze kubaki Uislamu na dini yao. Vivyo hivyo ni lazima kwa walimwengu wote katika majini na watu, waarabu na wasiokuwa waarabu wamwabudu Allaah pekee na wajisalimishe kwa yale aliyokuja nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Yeye ni Mtume wa Allaah wa haki na ndiye mwisho wa Manabii. Allaah amemtuma kwa watu wa ulimwenguni kote katika majini na watu, waarabu na wasiokuwa waarabu na nyumati zote. Ni lazima kwao wamwabudu Allaah na wajisalimishe na yale aliyokuja nayo Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Allaah (Subhaanah) amesema hali ya kuwa ni mwenye kumwamrisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) awafikishie watu:

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا

“Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote.”[17]

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا

”Hatukukutuma isipokuwa kwa watu wote na uwe mbashiriaji na muonyaji.”[18]

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ

“Hatukukutuma isipokuwa ni rehema kwa walimwengu.”[19]

Kwa hivyo yeye ni Mtume wa Allaah kwenda kwa wote; majini na watu, waarabu na wasiokuwa waarabu, mayahudi na manaswara na wafursi na walimwengu wote katika majini na  watu. Ni lazima kwao wote wamwabudu Allaah, wampwekeshe, wamkhusishe kwa ´ibaadah na wala wasiabudu mwengine pamoja Naye. Ni mamoja kiumbe hicho ni Malaika aliyekurubishwa wala Mtume aliyetumilizwa, mti, maiti, sanamu, mzimu wala chengine chochote. Ni lazima kwao wamkhusishe Allaah kwa ´ibaadah pasi na vyengine vyote. Ni lazima kwao wajisalimishe na yale aliyokuja nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wamtumie kama hakimu kati yao na wasitoke nje ya uongofu na njia yake. Amesema (Subhaanah):

فَلَا وَرَبِّكَ لَا يُؤْمِنُونَ حَتَّىٰ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لَا يَجِدُوا فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُوا تَسْلِيمًا

“Naapa kwa Mola wako! Hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni hakimu katika yale wanayozozana kati yao kisha wasipate katika nyoyo zao uzito katika yale uliyohukumu na wajisalimishe kwa kujisalimisha.”[20]

قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ ۖ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ ۖ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا ۚ وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ

”Sema: ”Mtiini Allaah na mtiini Mtume, mkigeukilia basi hakika jukumu lake ni lile alilobebeshwa nanyi ni juu yenu yale mliyobebeshwa; na mkimtii mtaongoka na hapana juu ya Mtume isipokuwa ufikishaji wa wazi.”[21]

فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ ۙ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ

“Basi wale waliomuamini na wakamtukuza na wakamnusuru na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye, hao ndio wenye kufaulu.”[22]

Hawa ndio waliofaulu. Ni wale waliomfata Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kuhusu waliotoka nje ya dini ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), hawakunyenyekea Shari´ah Yake na hawakumsadikisha, basi hawa ndio wakhasirikaji, waangamivu, wapotofu na makafiri pasi na kujali watakuwa na jinsia yao. Amesema (Subhaanah):

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا

“Sema: “Hakika mimi ni Mtume wa Allaah kwenu nyinyi nyote.”[23]

Akafanya uongofu unapatikana katika kumfuata. Kwa hivyo ikajulisha kwamba anayetoka nje ya Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) basi amekhasirika, amepotea na si mwongofu. Uongofu na kufaulu kunapatikana kwa kumfuata Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), katika kumtakasia ´ibaadah Allaah pekee, kuhukumiana na Shari´ah ya Allaah ambayo amekuja nayo Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa haya inapata kufahamika kwamba kilicho cha lazima kwa watu wote ni kumwabudu Allaah pekee na wamtakasia Yeye nia. Aidha ni lazima kwa nchi zote kumwabudu Allaah, kuwalazimisha raia wake kumwabudu Allaah na waache  yale wanayofanya ya shirki na ya upotofu. Haya ni yenye kuzienea nchi zote na watu wote. Lakini waislamu wenye kujinasibisha na Uislamu wajibu kwao ni kwa njia maalum na kubwa. Kwa sababu ni wenye kujinasibisha na dini ya Allaah na ni lazima kwao kuihakiki dini ya Allaah, waitukuze dini ya Allaah, wailinde na yale aliyoharamisha Allaah na wamtakasie ´ibaadah Allaah pekee ili uhakikike Uislamu wao na wawe waislamu wakweli na si wa kujinasibisha. Kujinasibisha hakusaidii na hakunufaishi kitu. Bali ni lazima Uislamu wao uwe wa kweli na kumwabudu Allaah pekee, wamtakasie Yeye nia, watukuze maamrisho na makatazo Yake, kumfuata Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ni lazima kwa mataifa mengine yasiyojinasibisha na Uislamu kama vile mayahudi, manaswara, waabudia moto na wengineo wasiomfuata Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wamwabudu Allaah pekee, wajisalimishe na Shari´ah aliokuja nayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ni lazima kwao wote walazimiane na mambo hayo. Kwa sababu wameamrishwa na wameumbwa kwa ajili ya mambo hayo. Allaah amemtuma Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwenda kwa walimwengu wote katika majini na watu. Kwa hivo haijuzu kwa yeyote katika wao kutoka nje ya Shari´ah ya Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yeyote awate.

[1] al-Bukhaariy (1864) na Muslim (1397).

[2] Muslim (976).

[3] Muslim (974).

[4] 10:18

[5] 39:03

[6] 01:05

[7] 17:23

[8] 04:35

[9] 39:02-03

[10] 72:18

[11] 16:36

[12] 21:25

[13] 51:56

[14] 31:08

[15] 52:17

[16] 15:45

[17] 07:158

[18] 34:28

[19] 21:107

[20] 04:65

[21] 24:54

[22] 07:157

[23] 07:158

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tahdhiyr min Fitnat-il-Qubuur, uk. 41-54
  • Imechapishwa: 21/04/2022