10. Israa´ na Mi´raaj


Kutokana na maoni sahihi ya wanachuoni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipandishwa katika safari ya usiku kutoka kwenye msikiti mtakatifu na kwenda Jerusalemu kwa roho na mwili wake. Alikuwa amepanda Buraaq huku akiongozana na Jibriyl (´alayhis-Salaam). Akashuka Jerusalemu na akawaongoza Mitume katika swalah.

Usiku huo huo akapanda kutoka sehemu hiyo kwenda mbingu ya dunia, kisha mbingu ya kufuata, kisha mbingu ya tatu, halafu mbingu ya nne, kisha mbingu ya tano, halafu mbingu ya sita kisha mbingu ya saba. Mbinguni aliwaona Mitume. Kisha akapandishwa mpaka kwenye mkunazi wa mwisho. Huko alimuona Jibriyl katika umbile ambalo Allaha amemuumba kwalo. Usiku huo Allaah alifaradhisha swalah.

Wanachuoni wametofautiana kama (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola Wake au hapana. Imesihi kupokelewa kutoka kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba amesema:

“Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimuona Mola Wake.”

Katika upokezi mwingine amesema:

“Amemuona kwa moyo wake.”

al-Bukhaariy na Muslim wamepokea ya kwamba ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alimkatalia mwenye kusema hivo. Yeye na Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) wamesema:

“Alimuona Jibriyl.”[1]

Muslim amepokea katika “as-Swahiyh” yake kupitia Qataadah kutoka kwa ´Abdullaah bin Shaqiyq ambaye ameeleza kuwa Abu Dharr amesema:

“Nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Je, ulimwona Mola Wako?” Akasema: “Ilikuwa ni nuru; vipi nitamwona.”[2]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Niliona nuru.”[3]

Hadiyth hii ni yenye kutosheleza juu ya maudhui hii.

Asubuhi yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawaeleza watu wake ishara kubwa ambazo Allaah amemuonesha. Wakazidi kumkadhibisha na kumuudhi zaidi.

Katika mnasaba wa Hajj Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akizungumza na makabila na kusema:

“Ni nani awezae kunichukua kwa watu wake na kunilinda ili niweze kufikisha ujumbe wa Mola Wangu? Hakika Quraysh wamenizuia kuweza kufikisha ujumbe wa Mola Wangu.”[4]

Wakati huo ami yake Abu Lahab (Allaah amlaani) alikuwa amesimama nyuma yake na kuwaambia watu:

“Msimsikize huyo! Ni mwongo!”

Makabila ya kiarabu yalikuwa yakimkwepa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wanaposikia jinsi Quraysh wanavyomtuhumu ya kwamba ni mwongo, mchawi, kuhani, mshairi na uwongo mwingine wanaojizushia kutoka kwao. Watu wa makabila wasioweza kuyapambanua mambo walikuwa wanawasikiliza. Lakini werevu pindi wanaposikia maneno yake na kuyafahamu, wanashuhudia kuwa anayoyasema ni haki na kwamba hao wengine wanamsemea uongo. Hivyo wanasilimu.

[1] al-Aajuurriy (491). Nzuri kwa mujibu wa ´Allaamah al-Albaaniy katika ”Dhilaal-ul-Jannah” (439).

[2] Muslim (178).

[3] Muslim (178).

[4] Ahmad (3/322).

  • Mhusika: Imaam Ismaa´iyl bin Kathiyr ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Fusuwl fiy Siyrat-ir-Rasuwl, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 18/03/2017