2 – Kuhusu mwanamke kutia rangi nywele zake, zikiwa ni mvi, basi azibadilishe kwa rangi nyingine isiyokuwa nyeusi. Hayo ni kutokana na ueneaji wa makatazo yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wa kupaka rangi nyeusi. Imaam an-Nawawiy amesema katika “ar-Riyaadh as-Swaalihiyn”:

“Mlango unaozungumzia makatazo kwa mwanaume na mwanamke kutia rangi nyeusi.”[1]

Vilevile amesema katika “al-Majmuu´”:

“Inapokuja katika makatazo ya kupaka rangi nyeusi hakuna tofauti kati ya mwanaume na mwanamke. Haya ndio madhehebu yetu.”[2]

Ama kuhusu mwanamke kupaka rangi nywele nyeusi za kichwani mwake ili ziende katika rangi nyingine naona kuwa kitendo hicho hakijuzu. Sioni haja ya kufanya hivo. Kwa sababu rangi nyeusi kwa nywele ndio uzuri na sio muumbuko unaohitajia kubadilishwa. Jengine ni kwa sababu kufanya hivo ni kujifananisha na wanawake wa kikafiri.

Ni halali kwa mwanamke kujipamba kwa dhahabu na fedha kwa mujibu wa desturi. Kuna maafikiano ya wanachuoni juu ya hilo. Lakini hata hivyo haijuzu kwake kuyaonyesha mapambo yake mbele ya wanaume ambao si Mahram zake. Bali anapaswa kuyafunika na khaswa pindi anapotoka nje ya nyumba yake na asiwaonyeshe nayo wanaume. Kwani kitendo hicho ni fitina. Hakika mwanamke amekatazwa kuwasikilizisha wanaume mlio wa mapambo yake yaliyoko mguuni mwake ndani ya nguo. Amesema (Ta´ala):

وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ

“Wala wasiodhihirishe mapambo yao.”[3]

Vipi kuhusu mapambo yanayoonekana?

[1] Uk. 626.

[2] (01/324).

[3] 24:31

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tanbiyhaat, uk. 23
  • Imechapishwa: 23/10/2019