10. Hadiyth ya tatu na ya nne kuhusu kufunga safarini


Hadiyth ya tatu

3- Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Tulisafiri pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika mwezi wa Ramadhaan wakati ambapo kulikuwa na joto kali kiasi cha kwamba kuna ambao walikuwa wakiweka mkono kichwani kutokana na ukali wa joto. Hakuna kati yetu ambaye alikuwa amefunga isipokuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ´Abdullaah bin Rawaahah.”

Maana ya kijumla:

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka na Maswahabah zake Ramadhaan katika masiku ambapo kulikuwa na jua kali. Kutokana na jua kuwa kali hakuna katika wao ambaye alikuwa amefunga isipokuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Rawaahah al-Answaariy (Radhiya Allaahu ´anh). Licha ya ugumu uliokuwepo akafunga. Ni dalili inayoonyesha juu ya kujuzu kufunga safarini ijapokuwa hilo litaambatana pamoja na uzito usiomfikisha mtu katika maangamivu.

Hadiyth ya nne

4- Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa safarini ambapo akaona msongamano na mtu ambaye amefanyiwa kivuli. Akasema: “Mambo gani haya?” Wakasema: “Amefunga.” Akasema: “Sio katika wema kufunga safarini.”

Tamko la Muslim limekuja likisema:

“Jilazimieni na ruhusa ya Allaah ambayo amekuruhusini.”

Maana ya kijuma:

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa katika moja ya safari zake ambapo akawaona watu wamesongamana na alikuwepo mtu ambaye amefanyiwa kivuli. Alipowaulizia jambo lake wakamjuza kwamba amefunga na amefikia mpaka kiwango cha kufanyiwa kivuli. Ndipo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye ni mwingi wa huruma na mkarimu akasema:

“Kufunga safarini sio katika wema. Jilazimieni na ruhusa ya Allaah ambayo amekuruhusini.”

Hakusudii kwa ´ibaadah zenu mziadhibu nafsi zenu.

Faida zinazochukuliwa kutoka katika Hadiyth:

1- Inafaa kufunga safarini kama ambavyo inafaa vilevile kutendea kazi ruhusa.

2- Kufunga safarini sio wema. Shani ya mambo ni kwamba inaangusha wajibu.

3- Bora ni kutendea kazi ruhusa ya Allaah (Ta´ala) aliyowafanyia wepesi kwayo waja Wake.

Tofauti ya wanachuoni:

Wanachuoni wametofautiana juu ya kufunga Ramadhaan safarini. Kuna baadhi ya Salaf, kama vile az-Zuhriy na an-Nukha´iy, ambao wamelifanyia hilo ukali na wameonelea kwamba swawm ya msafiri haisihi. Ni jambo limepokelewa pia kutoka kwa ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf, Abu Hurayrah, Ibn ´Umar na ndio pia madhehebu ya Dhwaahiriyyah.

Wanachuoni wengi wakiwemo wale maimamu wane wameonelea kwamba inafaa kufunga safarini kama ambavyo inafaa vilevile kula.

Wale wa mwanzo wametumia hoja maneno Yake (Ta´ala):

فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖوَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Yule atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi basi afunge na atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika masiku mengine.” (02:185)

Kutumia kwako dalili hapa ni kwa njia ya kwamba Allaah hakuwafaradhishia isipokuwa wale walioshuhudia na akamfaradhishia mgonjwa na msafiri katika masiku mengine.

Pia yale yaliyopokelewa na al-Bukhaariy kupitia kwa Jaabir:

“Sio katika wema kufunga safarini.”

Wanachuoni wengi wametumia hoja zilizo na nguvu kukiwemo Hadiyth ya mlango:

Ya kwanza: Hadiyth ya Hamzah bin al-Aslamiy:

“Ukitaka funga na ukitaka kula.”

Ya pili: Hadiyth ya Anas:

“Tulikuwa tukisafiri pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na yule mwenye kufunga hakumkosoa yule ambaye hakufunga na yule ambaye hakufunga hakumkosoa yule ambaye amefunga.”

Ya tatu: Hadiyth ya Abud-Dardaa´ ambapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifunga na pia ´Abdullaah bin Rawaahah.

Wamezijibu hoja za wale wa mwanzo kwa kusema:

Kuhusian na Aayah yule ambaye kateremshiwa nayo alifunga baada ya kuteremka kwake. Hakika ndiye kiumbe ambaye ni mjuzi zaidi wa maana yake. Inawezekana maana yake sio hiyo mlioitaja.

Kuhusu maneno yake:

“Hao ndio waasi.”

uhalisia wa mambo ni kwamba yanawahusu watu ambao swawm ilikuwa nzito kwao. Baada ya hapo akafungua (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili nao waweze kumuiga, jambo ambalo hawakufanya. Ndipo akasema:

“Hao ndio waasi.”

kwa kuacha kwao kumuiga (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Ama kuhusu Hadiyth:

“Sio katika wema kufunga safarini.”

maana yake ni kwamba kufunga safarini sio katika wema ambao watu wanatakiwa kushindana. Kula kunaweza kuwa ndio bora kuliko kufunga ikiwa kuna uzito. Kama mfano kula kunamsaidia mtu katika Jihaad. Isitoshe Allaah anapenda zitendewe kazi ruhusa Zake kama anavochukia kuendewa maasi Yake.

Wale wanachuoni wengi ambao wanaona kuwa inafaa kufunga safarini wametofautiana ni lipi ambalo ni bora zaidi; kufunga au kula? Maimamu watatu, Abu Haniyfah, Maalik na ash-Shaafi´iy, wanaona kuwa kufunga ndio bora ikiwa mtu hatohisi uzito. Imaam Ahmad yeye anaona kuwa kuacha kufunga ndio bora ijapokuwa mfungaji hatohisi uzito. Sa´iyd bin al-Musayyib, al-Awzaa´iy na Ishaaq pia wanaonelea kuwa imependekezwa kuacha kufunga.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdullaah bin ´Abdir-Rahmaan al-Bassaam
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-´Allaam Sharh ´Umdat-il-Ahkaam, uk. (1/326-329)
  • Imechapishwa: 04/06/2018