Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

690- Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ambaye yatamshinda matapishi hakuna juu yake kulipa na ambaye atajitapisha basi alipe.”[1]

Wameipokea watano. Ahmad ameitia dosari na ad-Daaraqutwniy ameipa nguvu.

691- Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mwaka ulipofunguliwa mji wa Makkah Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka kuelekea Makkah katika Ramadhaan. Watu walikuwa wamefunga. Mpaka alipofika Kuraa´-ul-Ghamiym akaomba chombo cha maji. Akakinyanyua ili watu wapate kumuona kisha akakinywa. Baada ya hapo akaambiwa kuwa kuna watu waliofunga ambapo akasema: “Hao ni waasi. Hao ni waasi.”

692- Katika upokezi mwingine imekuja:

“Akaambiwa: “Baadhi ya watu swawm imekuwa ngumu kwao na wanasubiri waone utachofanya.” Ndipo akaomba chombo cha maji baada ya ´Aswr.”[2]

Ameipokea Muslim.

693- Hamzah bin ´Amr al-Aslamiy amesema:

“Ee Mtume wa Allaah! Nahisi nguvu za kufunga safarini. Nina dhambi?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ni ruhusa kutoka kwa Allaah. Yule mwenye kuitendea kazi amefanya vizuri na mwenye kupenda kufunga hakuna dhambi juu yake.”[3]

Ameipokea Muslim. Msingi wake ni kwa al-Bukhaariy na Muslim kupitia kwa ´Aaishah aliyesimulia kuwa Hamzah bin ´Amr alimuuliza.

MAELEZO

Msafiri afunge au afungue? Hadiyth zimefahamisha kuwa mtu ana khiyari ya kufanya atakacho, lakini ni kipi bora kufunga au kula? Ikiwa msafiri anahisi uzito basi bora kwake ni kula na kukubali ruhusa ya Allaah (´Azza wa Jall). Ikiwa hahisi uzito basi bora ni yeye kufunga, kwanza ni kwa sababu ya kumwigiliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), pia ni kuharakisha kuitakasa dhimma yake. Jengine ni kwamba mtu anapata wepesi pindi anapofunga pamoja na wengine. Kwa ajili hii utamuona mtu kama ana madeni ya Ramadhaan basi siku moja inakuwa kama mwezi mzima. Baadhi wanahitaji mwaka mzima kwa ajili ya kulipa deni la siku siku moja au siku mbili, kwa sababu ya uzito wa kulipa. Kwa ajili hiyo bora kwa msafiri ni kufunga muda wa kuwa hahisi uzito wa funga. Hata hivyo yuko na khiyari ya kufanya atakacho.

[1] Ahmad (2/498), Abu Daawuud (2380), at-Tirmidhiy (720), an-Nasaa’iy (3119) na Ibn Maajah (1676).

[2] Muslim (1114).

[3] al-Bukhaariy (1943) na Muslim (1121).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mukhtaswar ´alaa Buluugh-il-Maraam (2/414-418)
  • Imechapishwa: 24/04/2020