10. Dalili ya kwanza kwamba yule asiyeswali sio kafiri

Mtu akiuliza ni upi msimamo unaotakiwa kushikwa juu ya dalili zilizotumiwa na wale ambao hawaonelei kwamba asiyeswali ni kafiri, ninasema kuwa dalili hizo hazijasema kuwa mtu asiyeswali sio kafiri au kwamba ni muumini au kwamba hatoingia Motoni au kwamba ataingia Peponi na mfano wa hayo. Atayezizingatia basi ataona kuwa hazitoki katika mafungu mane na hakuna fungu hata moja linalopingana na dalili zinazotumiwa na wale wenye kusema kuwa ni kafiri.

Fungu la kwanza: Hakuna dalili kabisa juu ya masuala haya. Kwa mfano ni dalili inayotumiwa na baadhi yao kwa maneno Yake (Ta´ala):

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا

“Hakika Allaah hasamehi kushirikishwa na anasamehe yaliyo chini ya hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi hakika amebuni dhambi kuu.”[1]

Maneno ya Allaah:

“… yaliyo chini ya hayo… “

kunalengwa madhambi yaliyo chini ya shirki, na sio madhambi mengine kuliko shirki. Anayekadhibisha kitu kilichoelezewa na Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni kafiri na amejipelekea katika ukafiri usiosamehewa hata kama dhambi yake hiyo sio shirki.

Lau tutasema kuwa inalenga madhambi mengine kuliko shirki, basi Aayah hiyo ni yenye kuenea na inafanywa maalum kwa dalili zengine zinazotilia nguvu ukafiri. Ukafiri unaomtoa mtu katika Uislamu ni katika madhambi yasiyosamehewa hata kama itakuwa sio shirki.

[1] 04:48

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Hukm Taarik-is-Swalaah, uk. 13-14
  • Imechapishwa: 22/10/2016