10. Asili ya I´aanat-ul-Mustafiyd


Wakati wa likizo ya msimu wa kipwa nilifundisha kitabu hiki Riyaadh na Twaaif. Baadhi ya wanafunzi walikuwa wakirekodi darsa hizo wakishirikiana na studio. Baada ya kukimaliza na rekodi zake zikasambaa, ndipo nikatumiwa maombi mengi ya kukiandika kutoka kwenye kanda na kukifanya kuwa aina ya kitabu. Mwanzoni nilikuwa nakataa maombi hayo na kutoa udhuru kwa sababu tayari zipo fafanuzi nyingi na zenye kutosha, jengine ni kwamba hakuna jipya nililosema. Wakati yalipokithiri maombi, nikajiambia mwenyewe kwamba huenda kuna kheri katika kutimiza matakwa yao:

وَعَسَىٰ أَن تَكْرَهُوا شَيْئًا وَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَعَسَىٰ أَن تُحِبُّوا شَيْئًا وَهُوَ شَرٌّ لَّكُمْ

“Huenda mkalichukia jambo ilihali ni lenye kheri kwenu na huenda mkapenda jambo ilihali ni lenye shari kwenu.”[1]

Ndipo nikawaacha wazitoe kwenye kanda na kuziandika chini ya uangalizi wangu. Baada ya hapo nikaisafisha kwa kiasi cha uwezo wangu. Hivi sasa kiko mbele yako. Yale yote yaliyopatiwa utayopata ndani yake yanatokamana na Allaah na yale yote yaliyokosewa utayopata ndani yake basi yanatokamana na kasoro na mapungufu yangu. Utakuwa umefanya tendo jema endapo utanizindua na kunisaidia kurekebisha.

Namuomba Allaah aniongoze mimi na wale ambao walikuwa ni sababu ya kutoka kitabu hiki katika elimu yenye manufa na matendo mema. Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake.

[1] 02:216

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 16
  • Imechapishwa: 10/09/2019