14. ´Aqiydah sahihi juu ya karama za mawalii

Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanaamini karama za mawalii ambazo Allaah (Ta´ala) ametaka wafanye, jambo ambalo limetajwa katika Maandiko mengi. Kwa mujibu wao walii ni yule mwenye kutekeleza maamrisho ya Kishari´ah na akajiepusha na yale ambayo yamekatazwa kwa mujibu wa Shari´ah. Amesema (Ta´ala) kuhusu mawalii:

أَلَا إِنَّ أَوْلِيَاءَ اللَّـهِ لَا خَوْفٌ عَلَيْهِمْ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ

“Zindukeni! Hakika mawalii wa Allaah hawana khofu juu yao na wala hawatohuzunika, ambao wameamini na wakawa wanamcha Allaah.” (10:62-63)

Ili mtu awe sampuli hii ya mtu kunahitajika imani na uchaji Allaah.

Karama ni kitu chenye kwenda kinyume na mazowea ambacho Allaah (Ta´ala) huwafanya wachaji Allaah na waja waumini wakifanye. Mambo hayo yanawasaidia kufanya mambo ya kidini au ya kidunia. Lakini hata hivyo karama za mawalii hazifikii ile daraja ya miujiza ya Manabii na Mitume.

Miongoni mwa karama za mawalii wa Allaah ni kile kisa cha watu wa Pangoni, kisa cha Maryam (Radhiya Allaahu ´anhaa) pindi uchungu ulipompeleka katika shina la mtende ambapo akaamrishwa na Allaah kutikisa mashina yake na matunda yakawa yameanguka pembezoni mwake, kule Allaah kumruzuku kwa njia ya kwamba alikuwa akipata matunda ya majira ya baridi wakati wa joto na matunda ya majira ya joto wakati wa baridi, kisa cha ´Aaswif (ambaye alikuwa ni mwandishi wa Sulaymaan), kisa cha bwana ambaye Allaah alimfisha miaka mia halafu baada ya hapo akamuhuisha, kisa cha Jurayj, kisa ch watu watatu katika wana wa Israaiyl ambao walichukua hifadhi kwenye pango na jiwe likawa limeziba maingilio yao na mfano wa visa kama hivyo ambavyo ni vyenye kujulikana kwa wanachuoni na vimethibiti katika Qur-aan, Sunnah iliyothibiti au yaliypokelewa kutoka kwa Salaf au waliokuja baada yao.

Karama itaendelea kuwepo katika Ummah huu hadi Qiyaamah kisimame, kwa kuwa sababu yake ni imani na uchaji Allaah na hivyo vitu viwili vitaendelea kuwepo mpaka siku ya Qiyaamah.

Lakini ikiwa jambo lenye kwenda kinyume na mazowea linatoka kwa mtu, hiyo haina maana kuwa ni dalili yenye kuonesha wema, imani na uchaji Allaah wake. Katika hali hii ni lazima matendo yake kwanza yalinganishwe na Qur-aan na Sunnah ili kuangalia kama yanaafikiana navyo na kama anavifuata kidhahiri na kindani.

Miongoni mwa fadhilah za mawalii ni yale aliyopokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) anasema: “Yule mwenye kumfanyia uadui walii Wangu, basi Nitatangaza vita dhidi yake.”

  • Mhusika: Shaykh ´Abdus-Salaam bin Barjas
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Mu´taqad as-Swahiyh, uk. 87-89
  • Imechapishwa: 21/06/2020