Mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) amemalizia milango ya “Kitaab-ut-Tawhiyd” kwa mlango huu. Kwa sababu ndani yake kuna majina na sifa za Allaah. Kitaab-ut-Tawhiyd chote kinazungumzia Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah na yale yenye kuikamilisha na yenye kuipunguza na yenye kupingana nayo. Ili kitabu kikamilike ndio maana akataja majina na sifa za Allaah. Kwani Tawhiyd-ul-Uluuhiyyah ndani yake kuna Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah na ndani ya Tawhiyd-ur-Rubuubiyyah kuna imani ya kuamini majina na sifa za Allaah. Umetajwa kivyake kwa sababu wako wakinzani juu ya suala hili, kama mfano wa Jahmiyyah, Mu´tazilah na Ashaa´irah. Maimamu wameraddi I´tiqaad zao hivi kwa ukali na wakatunga vitabu vingi na Ruduud nyingi. Mfumo wao unayatokomeza majina na sifa za Allaah na isitoshe ni kufanya Ilhaad. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا ۖ وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ ۚ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

”Allaah ana majina mazuri mno, hivyo basi muombeni kwayo na waacheni wale wenye kupondoka katika kuyapotosha majina Yake, watalipwa yale waliyokuwa wakiyatenda.”[1]

Allaah amejithibitishia Mwenyewe majina na sifa kama mfano wa kusikia, kuona, uwezo, uhai, elimu, uso na mikono. Yeye (Subhaanahu wa Ta´ala) amejithibitishia sifa za ukamilifu. Yule mwenye kupinga majina ya Allaah amefanya Ilhaad  katika majina ya Allaah na ni miongoni mwa wale ambao Allaah amewakusudia pale aliposema (Ta´ala):

 وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ

“… waacheni wale wenye kupondoka katika kuyapotosha majina Yake.”

Bi maana chana nao na yapuuze maneno yao – kwa sababu yanapingana na Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa ajili ya kukamilisha “Kitaab-ut-Tawhiyd” ndio maana mtunzi wa kitabu (Rahimahu Allaah) akamalizia kitabu hiki kwa mlango huu.

[1] 07:180

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: I´aanat-ul-Mustafiyd bi Sharh Kitaab-it-Tawhiyd, uk. 653
  • Imechapishwa: 09/09/2019