Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

Allaah (Ta´ala) amesema:

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

“Leo Nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni kwenu Uislamu uwe ndio dini yenu.” (05:03)

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِن كُنتُمْ فِي شَكٍّ مِّن دِينِي فَلَا أَعْبُدُ الَّذِينَ تَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَـٰكِنْ أَعْبُدُ اللَّـهَ الَّذِي يَتَوَفَّاكُمْ

“Sema: “Enyi watu! Ikiwa mna shaka kutokana na dini yangu, hivyo basi mimi siabudu ambavyo mnaviabudu badala ya Allaah; lakini namwabudu Allaah ambaye atakufisheni.” (10:104)

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اتَّقُوا اللَّـهَ وَآمِنُوا بِرَسُولِهِ يُؤْتِكُمْ كِفْلَيْنِ مِن رَّحْمَتِهِ وَيَجْعَل لَّكُمْ نُورًا تَمْشُونَ بِهِ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۚ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Enyi mlioamini! Mcheni Allaah na muaminini Mtume Wake! Hapo atakupeni sehemu mbili kati ya rehema Zake na atakujaalieni nuru mnatembea nayo na akusameheeni; Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” (57:28)

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mfano wenu nyinyi na watu wa Kitabu ni kama mfano mtu mwenye kukodisha wafanyakazi na akasema: “Ni nani katika nyinyi anayetaka kunifanyiakazi kuanzia asubuhi mpaka mchana kwa senti moja?” Mayahudi wakafanya hivo. Halafu akasema: “Ni nani katika nyinyi anayetaka kunifanyia kazi kuanzia mchana mpaka ´Aswr kwa senti moja?” Manaswara wakafanya hivo. Kisha akasema: “Ni nani katika nyinyi anayetaka kunifanyiakazi kuanzia ´Aswr mpaka jua kuzama kwa senti mbili?” Ndio nyinyi. Mayahudi na manaswara wakakasirika na kusema: “Ni kwa nini sisi ndio tufanye kazi sana na tupate malipo madogo?” Akasema: “Nimepunguza kitu katika malipo yenu?” Wakasema: “Hapana.” Ndipo akasema: “Hiyo ni fadhilah yangu ninampa yule ninayemtaka.”[1]

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Allaah amewapoteza waliokuwa kabla yetu siku ya ijumaa. Mayahudi wakapata jumamosi na manaswara jumapili. Allaah akatuleta na akatuongoza siku ya ijumaa. Kadhalika watatufuata siku ya Qiyaamah. Sisi ndio wa mwisho katika dunia hii, wa mwanzo siku ya Qiyaamah.”[2]

al-Bukhaariy amepokea kwa cheni ya wapokezi yenye kupungua kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Dini yenye kupendeza zaidi kwa Allaah ni ule upwekeshaji mwepesi.”[3]

Ubayy bin Ka´b (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Lazimianeni na Njia na Sunnah. Hakuna mja yeyote mwenye kulazimiana na Njia na Sunnah akamfikiria Allaah mpaka macho yake yakatiririka machozi kwa kumwogopa Allaah kisha akachomwa na moto. Hakuna mja yeyote mwenye kulazimianana na Njia na Sunnah akamfikiria Allaah mpaka mwili wake ukasisimka kwa kumwogopa Allaah isipokuwa mfano wake ni kama mfano wa jani kavu kwenye mti lenye kuruka hewani; hali kadhalika yanamtoka madhambi yake. Ni bora kuwa mkati na kati juu ya Njia na Sunnah kuliko kuwa na bidii katika yanayokwenda kinyume na Njia na Sunnah.”[4]

Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kule wale wenye busara wakawa ni wenye kulala na kuacha kufunga ni bora kuliko wajinga kuswali usiku na kufunga. Chembe kidogo ya wema ilio pamoja na uchaMungu na yakini, ni bora na ni yenye uzito zaidi kuliko ´ibaadah za waliodanganyika zilizo kubwa sawa na mlima.”[5]

[1] al-Bukhaariy (2268).

[2] al-Bukhaariy (876) na Muslim (855).

[3] al-Bukhaariy katika ”al-Adab al-Mufrad” (1/108).

[4] Ibn-ul-Mubaarak katika ”az-Zuhd” (1/21), Ahmad katika ”az-Zuhd” (1/196) na Abu Nu´aym katika ”Hilyat-ul-Awliyaa’” (1/252).

[5] Ahmad katika ”az-Zuhd” (137) na Abu Nu´aym katika ”Hilyat-ul-Awliyaa’” (1/211).

  • Mhusika: Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fadhwl-ul-Islaam, uk. 6-9
  • Imechapishwa: 23/10/2016