01. Utangulizi wa kitabu “Sharh Usuwl-is-Sittah”

Shaykh Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimhu Allaah) amesema:

Miongoni mwa ajabu ya maajabu na alama kubwa zenye kufahahamisha uwezo wa Mfalme mwenye kushinda ni misingi sita ambayo Allaah (Ta´ala) ameibainisha ubainifu wa wazi [kuwabainishia] watu wa kawaida wasiokuwa na elimu zaidi ya vile wanavyodhania wenye kudhania. Halafu baada ya haya wakakosea walimwengu wengi werevu na wenye akili isipokuwa wachache katika wachache.

MAELEZO

Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, ahli zake na Maswahabah zake wote.

Ni jambo lisilokuwa na shaka ya kwamba Allaah ameiteremsha Qur-aan hali ya kuwa ni yenye kubainisha kila kitu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akabainisha Qur-aan hii, ubainifu wenye kutosheleza. Kikubwa ambacho Allaah na Mtume Wake wamebainisha katika Qur-aan hii ni suala la Tawhiyd na shirki. Hili ni kwa sababu Tawhiyd ndio msingi wa Uislamu na msingi wa dini. Tawhiyd ndio ambayo kunajengwa juu yake matendo yote. Shirki inauvunja na kuuharibu msingi huu na unakuwa ni wenye kutokomea. Haya ni mambo mawili yenye kugongana na yaliyo kinyume ambayo hayawezi kamwe kukutana. Kwa ajili hiyo Allaah (Subhaanah) amebainisha msingi huu katika Kitabu Chake ndani ya Qur-aan nzima. Hukaribii kuvuka Suurah hata moja isipokuwa imetaja Tawhiyd na shirki.

Watu wanasoma Qur-aan hii na kuirudirudi. Hata hivyo ni wachache wenye kuzinduka na ubainifu huu. Ndio maana utaona watu wengi wanaisoma Qur-aan lakini wanatumbukia ndani ya shirki na wanaitia kasoro Tawhiyd. Pamoja na kwamba mambo haya yako wazi katika Kitabu cha Allaah na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wanafanya hayo kwa sababu ya kuwafuata wakale; mababu na Mashaykh zao. Msingi kwao umejengwa kwa kufuata yale waliyowakutaemo mababu, Mashaykh na watu wa mji wao. Hakuna siku miongoni mwa siku watafikiri kuiwekea Qur-aan mazingatio ili watambue yale waliyomo watu ni sahihi au sio sahihi. Badala yake wamewafuata kichwa mchunga mababa na mababu zao na kuchukulia kuwa Qur-aan inasomwa kwa ajili ya kutafuta baraka na ili mtu aweze kupata thawabu kwa kule kuisoma. Malengo si kwamba inasomwa kwa ajili ya kuizingatia na kuitendea kazi. Ni watu wachache mno wanaosoma Qur-aan kwa malengo haya. Badala yake wanasoma kwa ajili ya kutafuta baraka, kuburudika na sauti ya msomaji au kwa ajili ya kuwaponya nayo wagonjwa. Ni watu wachache miongoni mwa watu wanaosema hebu tuisome kwa ajili ya kuitendea kazi na kuzingatia yale yaliyomo na kuachana na yale waliyomo watu. Hatusemi kuwa hakuna wenye kufanya hivo, hata hivyo ni wachache mno. Kwa ajili hiyo ndio maana utaona kuwa Qur-aan iko upande huu na matendo yanayofanywa na baadhi ya watu yako upande mwingine. Kamwe hawafikirii kuleta mabadiliko.

Lau Mujaddid au mwenye kulingania katika dini ya Allaah atajaribu kuleta mabadiliko wa yale waliyomo, basi watamsimamia kidete na kumtuhumu upotevu, kumkufurisha, kwamba ameleta dini mpya na kadhalika. Hayo yalimtokea Shaykh huyu mwenyewe. Wakati (Rahimahu Allaah) alipojaribu kuwarudisha watu katika mafunzo ya Qur-aan na kubadili zile desturi na ufuataji kichwa mchunga waliyokuwemo, walimsimamia kidete na kumtia ndani ya uzushi na kwamba ni mtenda madhambi. Bali walifikia hata kumkufurisha na kumtuhumu tuhuma tele. Lakini ukweli wa mambo haya hayadhuru na si mepya. Mitume waliambiwa makubwa zaidi kuliko hayo. Wakati walipokuja na kutaka kubadili yale mambo ya kuabudia asiyekuwa Allaah ambayo watu walikuwemo, kulisemwa juu yaliyosemwa. Tusemeje juu ya walinganizi na wanazuoni? Kwa hiyo hili si jipya. Hili halipunguzi kitu katika ujira wa mwanachuoni na mlinganizi anayelingania katika dini ya Allaah. Yale wanayosema juu yao hayawadhuru kitu. Kinyume chake haya yanafanya mema yake kuzidi mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Madhara yanarudi kwa yule mwenye kumsema vibaya na kumchafua. Kuhusiana na wanazuoni wenye kumtakasia nia Allaah na wale walinganizi wanaolingania katika dini ya Allaah, yanayosemwa juu yao hayawadhuru kitu. Kinyume chake daraja na mema yao yanazidi.

Wanazuoni na walinganizi wana ruwaza njema kwa Mitume na yale yaliyosemwa juu yao na tuhuma walizotuhumiwa. Allaah (Ta´ala) amesema kuhusu Mtume Wake:

مَّا يُقَالُ لَكَ إِلَّا مَا قَدْ قِيلَ لِلرُّسُلِ مِن قَبْلِكَ ۚ إِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍ وَذُو عِقَابٍ أَلِيمٍ

“Huambiwi isipokuwa yaleyale waliyokwishaambiwa Mitume kabla yako. Hakika Mola Wako ni Mwenye msamaha na Mwenye adhabu iumizayo.” (41:43)

Shaykh (Rahimahu Allaah) katika kijitabu hiki atabainishia machache katika jambo hili la ajabu ya kwamba watu wanasoma Qur-aan, wanakithirisha kuisoma, wanaisoma yote mwanzo mpaka mwisho, wanaihifadhi, wanaisoma ipasavo na wanatilia umuhimu kusoma Qur-aan kwa Tajwiyd, jambo ambalo ni zuri. Lakini pamoja na hivyo makusudio sio haya. Makusudio ni mtu azingatie maana yake, aweke fikira zake katika Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall), ayapime matendo ya watu na Kitabu cha Allaah na kuangalia kama yanaenda sambamba nacho au yanaenda kinyume nacho? Hili ndilo linalotakikana kwa sisi tujirekebisha na kuwazindua watu juu ya makosa yao. Makusudio sio kuwakashifu na kuwaponda watu. Bali makusudio iwe ni kutengeneza na kuwatakia kheri.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sittah, uk. 05-08
  • Imechapishwa: 18/05/2021