1- Muslim amepokea kupitia kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hawatoacha kuomba watu kati yenu mpaka wakutane na Allaah pasina kuwa na nyama yoyote nyusoni mwao.”[1]

2- Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtu hatoacha kuwaomba watu mpaka akutane na Allaah siku ya Qiyaamah ilihali hana kinofu cha nyama usoni mwake.”[2]

Imepokelewa na al-Bukhaariy.

Hadiyth inaweza kufasiriwa kwa njia mbili:

1- Halisia, nayo ni kwamba mtu ambaye amefanya kuomba ndio kazi [yake]. Huyu anawaomba watu badala ya kumuomba Allaah. Atafanya vivyo hivyo siku ya Qiyaamah baada ya nyama zake za usoni kukatwa-katwa na kuwa kama fuvu.

2- Maana yake ni kwamba atakuja siku ya Qiyaamah hali ya kuwa hana heshima wala hadhi mbele ya Allaah (Ta´ala). Namna hii ndivyo ilivyopokelewa katika baadhi ya mapokezi na kwamba atakuja kwa Allaah na hana hadhi yoyote Kwake.

Inawezekana kuoanisha zote mbili na kusema kwamba atakuja na uso uliochubuka hali ya kuwa hana hadhi yoyote ikiwa hii ni nyongeza ya adhabu na Allaah ndiye Anajua zaidi.

[1] Muslim (1040) na Ahmad (4638).

[2] al-Bukhaaariy (1474), Muslim (1040) na an-Nasaa´iy (5/94).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad al-Qurtwubiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qam´-ul-Hirsw biz-Zuhd wal-Qanaa´ah, uk. 14
  • Imechapishwa: 18/03/2017