Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amesema:

”Tunaamini kuwa misingi ya Sunnah ni kushikamana barabara na mfumo wa Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuwaiga.. “

MAELEZO

Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Maneno haya yanayonasibishwa kwa Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) yanabainisha ´Aqiydah sahihi na ulinganizi katika ´Aqiydah ambayo ni wajibu kwa kila muislamu wa kiume na wa kike kushikamana nayo barabara. Ametaja (Rahimahu Allaah) kwamba msingi wa ´Aqiydah ambayo ni ya lazima ni kushikamana na yale waliyokuwemo wema waliotangulia. Wanafunzi wanatambua kuwa ´Aqiydah waliokuwemo Salaf inahusiana na kushikamana barabara na Qur-aan na Sunnah na hukumu zake zote za Kishari´ah, maamrisho na makatazo na mabainisho ya yaliyo ya halali na ya haramu.

Inapokuja katika majina na sifa za Allaah (Tabaarak wa Ta´ala), wanazithibitisha kwa njia inayolingana na ukubwa na utukufu wa Allaah, kama zilivyotajwa katika Qur-aan, Sunnah na zilivyofasiriwa na Salaf (Rahimahumu Allaah).

Katika milango mingine yote ya elimu na matendo yule wamuigaye ni Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye Maswahabah walichukua elimu kutoka kwake. Wakaifikisha kwa Taabi´uun waliokuja baada yao na wao pia wakaifikisha kwa wale waliokuja baada yao. Namna hii elimu iliendelea kuwa yenye kuhifadhiwa, mwadilifu kwenda kwa mwingine, mpaka hii leo.

Kitu muhimu zaidi ambacho Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanatilia umuhimu ni elimu kuhusu majina na sifa za Allaah na mwenendo wa kimatendo kama watangu wao.

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“… na kuwaiga… “

Uhakika wa mambo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye anayetakiwa kufuatwa. Kwa sababu wao ndio waliozungumza na Mtume wetu Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wakabeba ule Wahy wenye kuangaza kutoka katika Kitabu cha Allaah (´Azza wa Jall) na ubainifu maana zake pamoja na Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na ubainifu wa maana zake – katika kila mlango miongoni mwa milango ya elimu na maamrisho na makatazo yaliyokuja katika Uislamu na wakafaradhishiwa nayo watu.

Kuwaiga ni kuwashikamana barabara na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa sababu hawakugeuza wala kubadilisha kitu katika yale waliyoyasikia. Waliyaeleza, wakayatendea kazi na wakawafunza wengine. Waja wema walijifunza kutoka kwao, kama ilivyokuja katika mapokezi:

“Elimu hii itabebwa na kila mwema kutoka katika kila karne; wanailinda kutokamana na upotoshaji wa wajinga, dhana za watu wa batili na Bid´ah za wazushi.”

  • Mhusika: ´Allaamah Zayd bin Muhammad al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat al-Latwiyfah ´alaa Usuwl-is-Sunnah al-Muniyfah, uk. 17-18