1. Fadhilah za kusimama nyusiku za Ramadhaan

[1] Kumekuja Hadiyth mbili juu ya jambo hili.

Ya kwanza: Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akipenda kusimama nyusiku za Ramadhaan pasi na kuwaamrisha. Halafu akawaambia:

“Atakayesimama nyusiku za Ramadhaan pamoja na imamu kwa imani na matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akafariki na hali bado ikaendelea kuwa hivyo[1]. Kisha hali ikaendelea kuwa hali kadhalika katika ukhaliyfah wa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) na vivyo hivyo mwanzoni mwa ukhaliyfah wa ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh).”[2]

Ya pili: ´Amr bin Murrah al-Juhaniy amesema:

“Kuna mwanamume kutoka Qudhwaa´ah alikuja kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: “Ee Mtume wa Allaah! Unaonaje lau nitashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba wewe ni Mtume wa Allaah, nikaswali vipindi vitano, nikafunga mwezi, nikasimama nyusiku za Ramadhaan na nikatoa zakaah?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Atakayekufa katika hali hii, basi atakuwa ni katika wakweli na mashahidi.””[3]

[1] Bi maana Tarawiyh kutoswaliwa kwa mkusanyiko.

[2] Muslim na wengineo. Imetajwa katika “al-Irwaa´” (04/14/906) na “Swahiyh Abiy Daawuud” (1241) – namuomba Allaah anisahilishie kukikamilisha na kukichapisha. Na kuhusu taaliki ya ndugu Zuhayr kwenye kitabu changu “Swalaat-ul-´Iydayn”, uk. 32: “Allaah amemrahisishia mwalimu wetu al-Albaaniy kuchapisha sehemu ya kwanza ya “Swahiyh Abiy Daawuud”, ninaapa kwa Allaah sijui ameyatoa wapi. Sehemu ya kwanza iko kwangu na sijampa yeyote idhini ya kuikopi, kuichapisha wala kuisambaza. Hali kadhalika yale aliyoyataja mwaka 1403 katika chapa ya nne ya kitabu changu “at-Tawassul”, uk. 22, na kwamba mujaladi wa tatu wa “Silsilah al-Ahaadiyth adh-Dhwa´iyfah” umeshatoka. Leo ni tarehe 1406 Rajab na bado mpaka sasa hakijatoka!

[3] Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan katika “as-Swahiyh” zao na wengineo. Mlolongo wa wapokezi ni Swahiyh. Tazama taaliki yangu ya “Ibn Khuzaymah” (03/340/2262) na “Swahiyh at-Targhiyb” (01/419/993).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Qiyaam Ramadhwaan, uk. 17-18
  • Imechapishwa: 07/05/2019