Himdi zote anastahiki Allaah. Tunamhimidi Yeye, kumuomba msaada, kumuomba uongofu, kumuomba msamaha na kutubia Kwake. Tunajilinda kwa Allaah kutokamana na uovu wa nafsi zetu na matendo yetu maovu. Yule mwenye kuongozwa na Allaah, basi hakuna wa kumpoteza, na yule mwenye kupotezwa na Allaah, basi hakuna wa kumwongoza. Ninashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika, na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake – swalah na salaam ziwe juu yake.

Amma ba´d:

Tambueni – Allaah akurehemuni – ya kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameufadhilisha mwezi wa Ramadhaan juu ya miezi mingine yote kwa kuwa ndani yake ndio kateremsha Qur-aan. Inasemekana vilevile kuwa vitabu vilivyotangulia viliteremshwa katika Ramadhaan, lakini vitabu hivyo viliteremshwa mara moja. Kuhusu Kitabu chetu kiliteremshwa kwenye nyumba ya Nguvu katika mbingu ya dunia. Hivyo ndivyo Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alivyopokea. Kutoka kwenye nyumba ya Nguvu akateremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hatua kwa hatua. Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَقُرْآنًا فَرَقْنَاهُ لِتَقْرَأَهُ عَلَى النَّاسِ عَلَىٰ مُكْثٍ وَنَزَّلْنَاهُ تَنزِيلًا

“Qur-aan Tumeigawanya sehemu mbalimbali ili uwasomee watu kwa kituo na tumeiteremsha mteremsho wa kidogo kidogo.”[1]

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameeleza ya kwamba ameiteremsha Qur-aan kwa mja na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hatua kwa hatua. Amesema katika Aayah ya “al-Furqaan”:

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا نُزِّلَ عَلَيْهِ الْقُرْآنُ جُمْلَةً وَاحِدَةً ۚكَذَٰلِكَ لِنُثَبِّتَ بِهِ فُؤَادَكَ ۖوَرَتَّلْنَاهُ تَرْتِيلًا

“Wakasema wale waliokufuru: “Kwa nini hakuteremshiwa Qur-aan   kwa ujumla mara moja tu?” Hivyo ndivyo [Tunavyoiteremsha kidogo kidogo ni] ili Tukithibitishe kifua chako na Tumeipangilia kwa vituo na fasili bayana.”[2]

Allaah ameiteremsha kwa mja na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hatua kwa hatua kutegemea na matukio. Kila makafiri walipokuwa wakija na utata, Allaah (´Azza wa Jall) alikuwa akiwaraddi ndani yake. Kila ambapo makafiri walikuwa wakisema maneno, Allaah (´Azza wa Jall) akiwaraddi ndani yake. Kila wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiulizwa juu ya kitu, Allaah (´Azza wa Jall) anamjibu yule muulizaji. Mara mayahudi wakiuliza kuhusu roho, mara wakiuliza kuhusu mambo mengine. Kadhalika washirikina waliuliza maswali. Kwa msemo mwingine ni kwamba Allaah aliiteremsha mara moja kwenye nyumba ya Nguvu katika usiku wa Qadar Ramadhaan. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ فَمَن شَهِدَ مِنكُمُ الشَّهْرَ فَلْيَصُمْهُ ۖ وَمَن كَانَ مَرِيضًا أَوْ عَلَىٰ سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ

“Mwezi wa Ramadhaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo la batili. Basi atakayeshuhudia miongoni mwenu mwezi mpya na afunge . Atakayekuwa mgonjwa au safarini basi atimize idadi katika siku nyinginezo.”[3]

[1] 17:106

[2] 25:32

[3] 02:183-185

  • Mhusika: ´Allaamah Ahmad bin Yahyaa an-Najmiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Istiqbaal Shahri Ramadhwaan, uk. 21-23
  • Imechapishwa: 09/06/2017