1. Dibaji ya “Sharh Usuwl-is-Sunnah”

Himdi zote ni za Allaah. Tunamhimidi na kumuomba msaada na msamaha. Tunajikinga Kwake kutokana na shari ya nafsi zetu na matendo yetu maovu. Yule mwenye kuongozwa na Allaah, basi hakuna awezae kumpoteza, na yule mwenye kupotezwa na Allaah, basi hakuna awezae kumwongoza. Ninashuhudia ya kwamba hapana mola wa haki isipokuwa Allaah na ninashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake. Allaah amsifu na amswalie yeye, kizazi chake na Maswahabah zake.

Hakika ´Aqiydah ya Kiislamu iliyoletwa na nyujumbe zote ina nafasi kubwa katika Uislamu. Ndio asli katika Uislamu na yenye kutofautisha kati ya Dini sahihi na isiyokuwa sahihi. Kutokana na hilo wanachuoni wa Kiislamu – wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah – wametilia umuhimu katika kubainisha ´Aqiydah hii, kuifafanua, kulingania kwayo na kuitetea. Kwa ajili hiyo wameandika vitabu mbali mbali na kiasi kikubwa wakakiweka ndani ya vitabu vingine. Wameandika kuhusu hilo vitabu vidogo na vikubwa. Baadhi yavyo ni:

1- as-Sunnah ya ´Abdullaah bin Ahmad

2- as-Sunnah ya al-Khallaal

3- as-Shari´ah ya al-Aajurriy

4- Sharh Usuwl I´tiqaad Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah ya al-Laalakaa´iy

5, 6 – al-Ibaanah al-Kubraa na al-Ibaanah as-Sughraa ya Ibn Battwah

Watu hawa watukufu walitambua ´Aqiydah ina hadhi na nafasi gani na kwamba yule mwenye kwenda kinyume na kitu katika vipengele vyake au misingi yake yuko khatarini. Upindaji huo unaweza kuwa kufuru, Bid´ah, upotevu na kadhalika. Kujengea juu ya hilo ni wajibu kwa mwanafunzi kutilia umuhimu wa kusoma ´Aqiydah hii na misingi iliyojengwa juu yake.

Pengine mnajua kuwa al-Bukhaariy ameweka katika “as-Swahiyh” yake mlango unaohusiana na imani, kushikamana bara bara na Qur-aan na Sunnah na Tawhiyd. Haya yote yanaonesha ni umuhimu mkubwa wa ´Aqiydah na misingi ya Uislamu.

Abu Daawuud ameweka katika kitabu chake “as-Sunan” mlango unaoitwa “as-Sunnah”. Uko mwishoni wa kitabu. Hapa neno “Sunnah” linalenga ´Aqiydah na Manhaj.

Muslim ana mlango unaoitwa imani kilicho na ´Aqiydah sawa na vitabu hivi vingine.

Miongoni mwa vijitabu vidogo vilivyoandikwa kubainisha ´Aqiydah hii ni pamoja na kitabu hichi kilichoandikwa na Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah), imamu wa Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Imamu huyu alikuwa ni jibali; jibali la Sunnah, imani, kuipa nyongo dunia na kumcha Allaah. Ndio maana alikuwa ni kigezo na mtihani wenye kupambanua Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah kutokana na Ahl-ul-Bid´ah wadh-Dhwalaal. Mpaka hii leo mfumo wake bado ni mtihani. Misingi aliyopigana kwa ajili yake na kuifuata bado ni mtihani kati ya watu mpaka hii leo. Mwenye kwenda kinyume nayo, amewekwa katika mtihani na Ahmad, mfumo wake na ´Aqiydah yake. Ahmad alikuwa ni mtihani. Yule mwenye kumsema vibaya amejitolea dalili kujithibitishia juu ya upotevu wake, uchafu wake na shari yake. Yule mwenye kumuadhimisha na kumheshimu basi watu walikuwa wakitambua kuwa ni katika Ahl-us-Sunnah. Kwa sababu Ahmad na wengine hawaadhimishwi na kuheshimiwa isipokuwa ni kwa sababu ya Sunnah. Si Ahmad, ash-Shaafi´iy, Maalik, al-Awzaa´iy au mwingine yeyote asingelipata cheo hichi katika Ummah na kuadhimishwa isipokuwa ni kwa sababu ya kushikamana kwao bara bara na Sunnah, kuiheshimu, kulingania kwayo na kuitetea.

Hivyo basi, kuweni na utambuzi wa thamani ya Sunnah. Kuweni na utambuzi wa ni kina nani Ahl-us-Sunnah na na ni hadhi gani walonayo. Shikamaneni nao na piteni nyanyo zao. Wako katika njia iliyonyooka; wanafuata Qur-aan, Sunnah na njia ya Maswahabah na khaswa makhaliyfah waongofu.

Shikamaneni na hili. Someni kijitabu hiki kidogo. Tutakipitia mbio mbio. Mihadhara hii hatutoingia kwa undani sana. Itatutosheleza – Allaah akitaka – kukipitia mbio mbio na kuweka baadhi ya tanbihi kwa kiasi na itakavyowezekana.

Ninamuomba Allaah atupe uelewa wa Dini Yake, atuthibitishe katika njia iliyonyooka, atuepushe sisi na nyinyi na njia za matamanio na upotevu na atunufaishe kwa kitabu hichi na vitabu vinginevyo vya Uislamu na khaswa vitabu vya ´Aqiydah; ´Aqiydah ya Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Usuwl-is-Sunnah, uk. 361-362
  • Imechapishwa: 18/03/2017