Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

Chuo cha maji

MAELEZO

Pindi wanachuoni wanazungumzia Fiqh huanza vitabu vyao kwa twahara. Hilo ni kwa sababu twahara imegawanyika aina mbili:

1- Twahara ya moyo.

2- Twahara ya mwili.

Twahara ya moyo ni ya kimaana na maana yake ni mtu ausafishe moyo wake kutokamana na shirki aina zote, Bid´ah zote na vifundo, chuki na hasadi juu ya waumini. Hii ndio twahara muhimu zaidi.

Twahara ya kimwili ni twahara ya kuinje na kinachokusudiwa ni mambo mawili:

1- Twahara kutokamana na hadathi.

2- Twahara kutokamana na najisi na uchafu (kama mfano wa mkojo na kinyesi).

Aina ya twahara ya kwanza inapatikana kwa kufuata Qur-aan na Sunnah na kuvidurusu ipasavyo.

Aina ya twahara ya pili inapatikana kwa maji. Kuhusu twahara kutokamana na najisi inafikiwa kwa maji na vyenginevo. Kila kinachoondosha najisi basi hiyo ni chenye kutwahirisha. Kinaweza kuwa maji, petroli na chenginecho. Ama twahara kutokamana na hadathi – ambayo ni ima kule kutawadha au kuoga – haiwi isipokuwa kwa maji peke yake. Kwa sababu Allaah wakati alipotaja wudhuu´ na kuoga akasema:

فَلَمْ تَجِدُواْ مَاء

“… na hakumpata maji… “[1]

Akafanya cha kujitwahirisha kwacho mtu ni maji.

Kwa ajili hii mtunzi wa kitabu ameandika mlango unaozungumzia aina mbalimbali za maji. Hapana shaka kwamba maji ni masafi, mengine yasiyokuwa na shaka ni ya najisi na ya tatu ni yale yenye kutatiza; je, ni ya najisi au ni masafi?

[1] 04:43

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mukhtaswar ´alaa Buluugh-il-Maraam (1/21-22)
  • Imechapishwa: 26/04/2020